KAMWE ASEMA MKOSA HAYANA NAFASI, YANGA YAPANIA TIKETI YA FAINALI
MSEMAJI wa Yanga, Ali Kamwe, amesema Azam FC inakabiliwa na mtihani mgumu katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB, akisisitiza kuwa malengo ya Wananchi ni kuhakikisha wanatinga hatua ya fainali ya michuano hiyo.
Yanga na Azam FC zinatarajiwa kukutana Junib21, 2026 , CCM Kirumba Mwanza mchezo ambao mkubwa na unalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wengi wa soka nchini, huku kila upande ukiwa na matarajio makubwa ya kusonga mbele na kuendelea kuwania taji hilo muhimu.
Akizungumza kuhusu mchezo huo, Kamwe amesema kuwa Yanga inaiheshimu Azam FC kutokana na ubora wa kikosi chake na kiwango ilichokionyesha katika mashindano mbalimbali msimu huu. Hata hivyo, alisisitiza kuwa heshima hiyo haitawazuia Wananchi kupambana kwa nguvu zote kutafuta ushindi.
“Hatua ya nusu fainali ni sehemu ambayo makosa hayana nafasi, kwani kila timu inapambana kutimiza ndoto ya kufika fainali na hatimaye kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB,” amesema .
Kamwe amesema maandalizi ya Yanga yanaendelea vizuri chini ya benchi la ufundi, huku juhudi zikifanyika kuhakikisha wachezaji wote wanaingia uwanjani wakiwa katika utimamu wa hali ya juu kimwili na kiakili kwa ajili ya mchezo huo muhimu.
Amebainisha kuwa historia ya mechi kati ya Yanga na Azam FC imekuwa na ushindani mkubwa kwa miaka mingi, jambo linaloongeza mvuto wa pambano hilo na kuwapa mashabiki matarajio ya kushuhudia mchezo wa kiwango cha juu.
Kamwe amewataka mashabiki wa Yanga kujitokeza kwa wingi kuisapoti timu yao, akieleza kuwa mchango wao kutoka jukwaani unaweza kuwa nguvu muhimu kwa wachezaji katika harakati za kutafuta ushindi na tiketi ya kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.