AZAM FC YASHIKILIA HATMA YA UBINGWA WA SIMBA
WAKATI mbio za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara zikifikia hatua ya mwisho, macho ya mashabiki wengi wa Simba yanaelekezwa katika mchezo wa kesho kati ya Azam FC na Yanga, ambao unaweza kuwa na mchango mkubwa katika kuamua hatma ya taji la msimu huu.
Mchezo huo utakaopigwa katika dimba la New Amaan Complex Zanzibar, ambapi Yanga watakuwa wenyeji.
Simba imeendelea kuweka matumaini yake hai baada ya kukusanya matokeo muhimu katika michezo yake ya hivi karibuni, jambo ambalo limeifanya ibaki kwenye ushindani wa karibu wa kuwania ubingwa huo.
Akizungumza kuhusu mbio hizo, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema matokeo ya mchezo wa Yanga dhidi ya Azam FC yanaweza kuipa Simba nafasi kubwa zaidi ya kusogea karibu na taji.
Ahmed amesema Azam FC tayari imeonyesha uwezo wake mkubwa baada ya kile ilichokifanya Mwanza, hivyo anaamini inaweza tena kuwa kikwazo kwa Yanga katika pambano hilo muhimu.
“Azam FC akiweza kufanya kile ambacho amekifanya Mwanza basi itakuwa ameturahisishia safari yetu ya ubingwa. Hivyo tunachohakikisha kwa sasa ni kushinda mechi zetu huku tukimuombea mabaya Yanga,” amesema Ahmed.
Kauli hiyo inaonyesha namna ambavyo Simba imejikita katika kuhakikisha inafanya kazi yake uwanjani huku ikisubiri matokeo yatakayoweza kuwapa faida katika mbio za ubingwa.
Iwapo Yanga itateleza katika mchezo huo wa kesho, Simba itakuwa imepata nafasi adhimu ya kujihakikishia njia nyepesi zaidi kuelekea kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania Bara, huku ushindani wa msimu huu ukiendelea kuwa mkali hadi dakika za mwisho.