Hersi Aionya Simba, Tano Sio Mwisho, Zingine Zinakuja
RAIS wa Yanga, Hersi Said, ameonekana kutuma ujumbe mzito kwa watani zao, Simba, akisisitiza kuwa endapo hawatajipanga vizuri wanaweza kuendelea kushuhudia Yanga ikitawala Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu mingi zaidi.
Hersi amesema kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tano mfululizo si mwisho wa mafanikio ya klabu hiyo, bali ni mwanzo wa safari ya kuongeza mataji zaidi katika misimu ijayo.
Amesema ana imani Yanga itaendelea kuwa nguvu kubwa katika soka la Tanzania kutokana na mipango madhubuti ya uongozi, uwekezaji katika kikosi chenye ushindani na dhamira ya kuendeleza mafanikio.
Akizungumza baada ya kutwaa taji hilo, Hersi alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa mafanikio hayo na kusisitiza kuwa bado wana malengo makubwa mbele yao.
“Alhamdulillah! Tano, jumlisha kadhaa zijazo Insha Allah,” amesema Hersi, akionesha imani kuwa Yanga itaendelea kuongeza idadi ya mataji ya Ligi Kuu katika misimu ijayo.
Kauli hiyo imezua mjadala mkubwa miongoni mwa wadau na mashabiki wa soka, huku wengi wakii tafsiri kama ishara ya kujiamini kwa uongozi wa Yanga kuhusu uwezo wa klabu hiyo kuendelea kubaki kileleni mwa soka la Tanzania.
Kwa upande mwingine, baadhi ya mashabiki wameiona kauli hiyo kama dongo kwa watani wao, Simba, ambao wamekosa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu mitano mfululizo.
Wakati Yanga ikifurahia mafanikio hayo, uongozi wa klabu unaendelea na maandalizi ya kuimarisha kikosi kwa ajili ya msimu ujao, ukiwa na lengo la kutetea ubingwa wa ligi na kufanya vizuri zaidi katika mashindano ya kimataifa.