Yanga SC

Yanga Wamtaka Akaminko Kuimarisha Safu Ya Kiungo

Vardo July 3, 2026 8:47 am

UONGOZI wa Yanga SC umeanza mazungumzo rasmi na kambi ya kiungo wa Azam FC, James Akaminko, katika harakati za kuimarisha kikosi chake kuelekea msimu wa 2026/27.

Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa kiungo huyo raia wa Ghana ameibuka miongoni mwa wachezaji wanaopewa kipaumbele na benchi la ufundi, ambalo linaamini ana uwezo wa kuongeza ubora, utulivu na ushindani katika safu ya kiungo.

Akaminko anatarajiwa kumaliza mkataba wake na Azam FC Julai 5 mwaka huu, hali inayomfanya kuwa miongoni mwa wachezaji wanaovutia kwenye dirisha la usajili endapo hataongeza mkataba na klabu yake ya sasa.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, Yanga ipo katika hatua za mwisho za kufanya tathmini ya usajili huo, huku mazungumzo kati ya pande hizo yakiendelea kwa lengo la kufikia makubaliano yatakayomnasa kiungo huyo.

“Hadi sasa hakuna makubaliano ya mwisho yaliyofikiwa, lakini mazungumzo yanaendelea vizuri. Kila upande unaendelea kujadili masharti mbalimbali ya dili hilo kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo hicho kiliongeza kuwa iwapo usajili huo utakamilika, Akaminko atakuwa miongoni mwa nyongeza muhimu zitakazoimarisha kikosi cha Yanga katika harakati za kutetea mataji ya ndani pamoja na kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya kimataifa msimu ujao.

Viongozi wa Yanga wanaamini uzoefu, uwezo wa kucheza katika nafasi mbalimbali za kiungo na utulivu alionao Akaminko vitakiongezea nguvu kikosi hicho, huku ushindani wa namba ukitarajiwa kuongezeka kuelekea msimu mpya wa 2026/27.

Simba Wajipa Kazi Moja Tu, Azam Fc Kazi Wanayo Dube Aibwaga Yanga Atimkia Hardrock FC