Simba Ipo Tayari Kuandika Historia CRBD, Barker
KOCHA Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesema kikosi chake kipo tayari kupambana kwa nguvu zote kuhakikisha kinatwaa Kombe la Shirikisho la CRDB Bank, akieleza kuwa ubingwa huo utakuwa zawadi kwa mashabiki pamoja na matunda ya kazi kubwa iliyofanywa na timu katika msimu mzima.
Barker amesema kufika hatua ya fainali ni mafanikio muhimu kwa Simba, lakini lengo lao halijaishia hapo, bali ni kuhakikisha wanamaliza safari hiyo kwa kutwaa taji.
Amesisitiza kuwa wachezaji wote wanaelewa uzito wa mchezo huo na wamejipanga kikamilifu kuingia uwanjani kwa ari ya ushindi.
Kocha huyo ameongeza kuwa maandalizi ya timu yamekamilika kwa kiwango kinachoridhisha, kuwa wachezaji wote, vijana na wenye uzoefu, wako katika hali nzuri ya ushindani na tayari kutoa mchango wao ili kufanikisha malengo ya klabu.
“Ubingwa wa kombe hili utakuwa zawadi yetu kwa juhudi ambazo tumezionesha katika msimu mzima,” alisema Barker.
Akizungumzia fainali dhidi ya Azam FC, Barker amesema anatarajia ushindani mkali kutokana na timu hizo kufahamiana vizuri baada ya kukutana mara kadhaa msimu huu. Hata hivyo, ameonyesha imani kuwa Simba itatumia vyema nafasi zitakazojitokeza ili kuibuka na ushindi.
Simba na Azam FC zinatarajiwa kuvaana kesho Julai 4, 2026, katika fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB Bank, uwanja wa Ngombani, Pemba huku Wekundu wa Msimbazi wakisaka kumaliza msimu kwa kutwaa taji hilo muhimu.