Bao La Zayd Laleta Tabasamu Simba, Yatwaa Ubingwa Shirikisho
SIMBA imetwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB Bank baada ya kuichapa Azam FC kwa bao 1-0 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Ngombani, Pemba, Zanzibar.
Bao pekee la ushindi lilipatikana dakika ya 62 baada ya beki wa Azam FC, Yahya Zayd, kujifunga alipokuwa akijaribu kuokoa mpira uliotokana na faulo iliyopigwa na kiungo Elie Mpanzu, na kuipa Simba bao lililodumu hadi mwisho wa mchezo.
Mchezo huo ulikuwa na ushindani mkubwa, huku kipindi cha kwanza kikimalizika kwa sare ya bila kufungana. Timu zote zilitengeneza nafasi kadhaa za kufunga, lakini washambuliaji wa pande zote walishindwa kuzitumia ipasavyo.
Dakika ya 68, Azam FC ilipata pigo baada ya kiungo wake, Feisal Salum ‘Fei Toto’, kuonyeshwa kadi nyekundu na mwamuzi Amon Sifa wa Mbeya kufuatia kumchezea vibaya Anicet Oura, jambo lililoifanya Azam kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji 10.
Ushindi huo umeifanya Simba kujifariji baada ya kukosa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliokwenda kwa watani wao, Yanga, kwa kutwaa taji la Kombe la Shirikisho.
Hili ni taji la pili kwa Simba msimu huu, baada ya awali kutwaa Kombe la Muungano kwa kuifunga Yanga, hivyo kuhitimisha msimu kwa makombe mawili na kurejesha tabasamu kwa mashabiki wa Wekundu wa Msimbazi.