Mtibwa: Tutarudi Na Nguvu Mpya
TUMEKUBALI. Ni kauli ya Beki na Nahodha wa Mtibwa Sugar, Erick Kyaruzi akielezea matokeo ya timu hiyo baada ya kushuka daraja, akisema wanasubiri mipango ya uongozi kuona wanajipangaje msimu ujao wa Ligi ya Championship huku matarajio yao ni kurudi na nguvu mpya.
Mtibwa Sugar imeshuka daraja ikiungana na KMC baada ya kukusanya pointi 27 na kumaliza nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ambapo msimu ujao itacheza Ligi ya Championship kujitafuta tena kurudi Ligi Kuu. Timu hiyo imeshuka daraja ikiwa na rekodi mpya Ligi Kuu baada ya kucheza mechi 15 za ugenini bila ushindi wowote, ikiwa ni sare sita na kupoteza nane.
Hii ni mara ya pili kwa timu hiyo kongwe nchini iliyowahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu misimu miwili mfululizo 1999 na 2000 kushuka daraja baada ya msimu wa 2023-2024.
“Ni matokeo ya mpira, hatukuwa na tatizo lolote aidha ndani au nje ya uwanja, lazima tukubali na kilichotokea na badala yake tusubiri mipango ya uongozi, ninaamini tutarudi tena Ligi Kuu,” amesema Kyaruzi.
Beki huyo aliyewahi kukipiga Kagera Sugar, ameongeza kuwa yapo ya kujifunza kwenye ligi iliyomalizika akiwaomba wadau na mashabiki wa timu hiyo kuungana kwa sasa ili kuirejesha tena Mtibwa Sugar Ligi Kuu.
“Wadau na mashabiki wasiwe mbali na timu licha ya kilichotokea bali tuungane kwa mawazo na ushauri kuona Mtibwa Sugar inarejea Ligi Kuu, naamini kipo cha kujifunza kuweza kujipanga upya,” amesema nyota huyo.