Simba SC

Simba, Azam Kusaka Heshima Pemba

Vardo July 4, 2026 7:54 am

BAADA ya kushuhudia Yanga ikibeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara ikiziacha Simba na Azam nafasi ya pili na tatu mtawalia, timu hizo zinasaka heshima leo ambapo filimbi ya mwisho itakapopulizwa, basi upande mmoja utakuwa na furaha na mwingine kilio.

Hilo litatokea kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba itakapopigwa fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ikizikutanisha timu hizo ambazo hazijawahi kukutana hatua hiyo, huku kila moja ikidai inabeba kombe na kurudi nalo Dar es Salaam.

Simba imetinga hatua hiyo ikitoka kuifanya ngazi Coastal Union baada ya kuichapa mabao 4-0 kwenye mchezo wa nusu fainali iliyopigwa Juni 20, 2026 kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Azam ilikata tiketi ya fainali ikiivua ubingwa Yanga kwenye mechi ya nusu fainali ya pili iliyopigwa Juni 21, 2026 katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, matajiri hao wa Dar es Salaam wakiibuka na ushindi wa mabao 3-2.

Timu zote zina kiu kubwa ya taji hilo likiwa ndilo pekee ambalo limesalia kulishindania msimu huu.

Simba inalitaka taji hilo kwa hesabu za kwenda kutuliza presha mashabiki wake baada ya kuukosa ubingwa wa Ligi Kuu ya NBC ulioendelea kusalia kwa watani zao, Yanga, kwa msimu wa tano mfululizo.

Ikiwa imeonyesha kiwango bora kwenye ligi kwa kuipiga presha kubwa Yanga, historia inaibeba Simba ikiwa na rekodi bora ya kushinda fainali ya michuano hiyo tangu kurejea kwake 2015, ikifanya hivyo mara tatu kwenye misimu ya 2016-2017 ilipoichapa Mbao FC mabao 2-1, ikarudia msimu wa 2019-2020 ilipoipiga Namungo kipigo kama hicho kisha kuichapa Yanga bao 1-0 msimu wa 2020-2021.

Mzimu wa kupoteza fainali upo Azam ikiwa imeshinda moja pekee ilipoichapa Lipuli bao 1-0 msimu wa 2018-2019, lakini ikapoteza mara tatu zote dhidi ya Yanga, ikikubali kipigo cha mabao 3-1 msimu wa 2015-2016, ikaiachia tena Yanga ubingwa msimu wa 2022-2023 kwa kipigo cha bao 1-0 na fainali ya mwisho kwao kupoteza ilikuwa 2023-2024 ikilikosa taji kwa mikwaju ya penalti 6-5.Kuonyesha inalihitaji taji hilo, Simba iliwapumzisha mastaa wengi bora wanaounda kikosi cha kwanza mchezo wa mwisho wa ligi dhidi ya KMC ilipomaliza msimu kwa ushindi wa bao 1-0.

Kocha Steven Barker, alishatangaza vita kuelekea fainali hiyo itakayoanza saa 11:00 jioni, akisema wataingia na akili moja tu uwanjani kuhakikisha wanalichukua taji hilo ili kuufunga msimu vizuri likiwa ni la pili kama watafanikiwa baada ya awali kulichukua lile la Muungano walipoifunga Yanga bao 1-0.

Tishio kubwa upande wa Simba chini Barker kwenda Azam ni kwamba haijapoteza mchezo wowote kwenye ligi wala mashindano hayo, kocha huyo akifanikiwa kurudisha kiwango bora cha Wekundu wa Msimbazi.

Jeuri ya Simba ni kwamba, ina ukuta mgumu ambao ulimaliza ligi ukiruhusu mabao 11 kwenye mechi 30 lakini pia ukiwa na safu bora ya kiungo na ile ya ushambuliaji ikifunga mabao 54.

Simba itawategemea viungo wake Elie Mpanzu ambaye sasa anatumika kama mshambuliaji wa mwisho, lakini pia Clatous Chama, Libasse Gueye na Anicet Oura ambao wamekuwa wakiwabeba Wekundu hao wa Msimbazi kwenye mechi za hivi karibuni.

Azam nayo haipo kinyonge ikitaka kufanya kweli kwa kulichukua taji hilo kwenda kuunogesha msimu wa 2025-2026 chini ya kocha aliyeweka rekodi tofauti kikosini hapo, Florent Ibenge.

Matajiri hao wa Chamazi msimu huu waligoma kupoteza dhidi ya Simba ikiwachapa mechi moja ya mzunguko wa kwaza wa ligi lakini ikatoa sare mchezo wa pili ikionyesha kwamba inawamudu Wekundu hao wa Msimbazi.

Azam ilifanya kilekile ikiwapumzisha wachezaji muhimu mchezo wa mwisho wa ligi ilipoichapa Dodoma jiji mabao 2-0 akiwemo staa Feisal Salum ‘Fei Toto’ bila kujali alikuwa anawania rekodi ya mfungaji bora, akiikosa na kwenda kwa mshambuliaji wa Singida Black Stars, Mosi Nduwumwe.

AZAM MAPEMA

Azam ilikuwa ya kwanza kutua Pemba kwaajili ya mchezo huo ikitumia usafiri wa boti, ikiwahi kuzoea hali ya hewa hapa kisiwani ikionyesha kwamba inalitaka taji hilo liwe la pili kwenye historia ya klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2004.

Wapinzani wao Simba wametua siku moja kabla ya mechi kwa ndege wakitokea moja kwa moja Dar es Salaam. Kabla ya kuanza kwa safari hiyo, kikosi hicho kilifanya mazoezi ya mwisho, kisha jana kujifua hapa Pemba kuanzia saa 12 jioni.

WAAMUZI HAWA HAPA

Fainali hii itachezeshwa na mwamuzi wa kati Sifu Amoni kutoka Mbeya akisaidiwa na Hamdani Said (Mtwara) na Zawadi Yusuph (Dar es Salaam) wakati Ahmed Arajiga kutoka Manyara akiwa mwamuzi wa akiba.

Siri Za Anubis Zafunguliwa Ili Uwe Mshindi Anayefuata Chilambo Afichua Jambo Kwa Ibenge