Simba SC

Simba Sc Yajipanga Upya, Kapombe Msimu Ujao Ni Moto

Vardo July 6, 2026 10:05 am

NAHODHA wa Simba SC, Shomary Kapombe, ameibuka na ujumbe mzito kwa mashabiki wa klabu hiyo akiahidi kuwa kikosi chao kitaendelea kujituma zaidi na kufanya makubwa msimu ujao wa mashindano, huku akishusha presha na kuwataka waendelee kuwa na imani na timu yao.

Kapombe ametoa shukrani za dhati kwa mashabiki wa Simba kwa sapoti kubwa waliyoonyesha wakati wa sherehe za ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB, ambazo zilijaa shamrashamra na furaha ya pamoja.

Amesema mapokezi makubwa waliyopewa tangu walipowasili Dar es Salaam hadi kufikia kilele cha gwaride la ubingwa katika Ufukwe wa Coco Beach ni ishara halisi ya mapenzi na uaminifu mkubwa ambao mashabiki wa Simba wanayo kwa klabu yao.

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Kapombe amesema kikosi kizima kimeguswa na mwitikio mkubwa wa mashabiki hao na kuahidi kutowaangusha.

“Kwa niaba ya wachezaji, kwanza tunapenda kuwashukuru mashabiki na wanachama wote ambao mmejitokeza kwa wingi. Hatukutarajia kuona umati mkubwa kama huu,” amesema Kapombe.

Amewataka mashabiki kuendelea kuwa bega kwa bega na timu hiyo kuelekea msimu ujao, akisisitiza kuwa sapoti yao ndiyo injini ya mafanikio ya Simba.

“Tunaomba jambo moja, kama mlivyokuwa nasi leo, msimu ujao muendelee kutusapoti kwa nguvu hizi hizi. Tukipata sapoti kama hii tunaamini tutafanya makubwa zaidi kuliko tuliyofanya msimu huu,” ameongeza.

Kapombe, ambaye amekuwa sehemu ya Simba tangu mwaka 2017, amesema wachezaji wote wamejipanga kuhakikisha wanapambana kwa nguvu zote ili kuipeperusha bendera ya klabu hiyo kwa mafanikio zaidi katika mashindano ya msimu ujao.

Vita Za Usajili Zaanza Kuchacha, Simba, Yanga Mtu Kati Nyota Sauz Julietha Singano Kutimkia Saudia