Vita Za Usajili Zaanza Kuchacha, Simba, Yanga Mtu Kati Nyota Sauz
UKIACHANA na ushindani wa ndani ya uwanja, sasa vita kati ya Simba na Yanga imehamia kwenye usajili, baada ya vigogo hao wa soka Tanzania kuingia kwenye mbio za kuwania saini ya winga wa Shekhukhune United ya Afrika Kusini, Keletso Makgalwa, kuelekea msimu wa 2026/27.
Taarifa zinaeleza kuwa Simba na Yanga zimeanza kufanya jitihada za kumnasa nyota huyo, kila mmoja ukilenga kuimarisha kikosi chake kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa mashindano.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Afrika Kusini, klabu hizo tayari zimeanzisha mawasiliano na Makgalwa, ambaye anaelezwa kuwa yupo tayari kutafuta changamoto mpya nje ya Shekhukhune United.
Winga huyo amevutia vigogo mbalimbali kutokana na kiwango chake bora, jambo lililozifanya Simba na Yanga kuonyesha nia ya dhati ya kupata saini yake ili kuongeza nguvu katika safu zao za ushambuliaji.
Hata hivyo, mazungumzo kati ya pande husika bado yanaendelea, huku kila klabu ikisaka kufikia makubaliano yatakayoiwezesha kumtambulisha nyota huyo kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili.
Iwapo usajili huo utakamilika, Makgalwa anatarajiwa kuwa miongoni mwa wachezaji watakaoongeza ushindani mkubwa katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu ujao, kutokana na uzoefu wake mkubwa alioupata katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini.