Kocha Wa Makombe Manqoba Mngqithi Atua Jangwani
BAADA ya Yanga kumtambulisha rasmi kocha mkuu mpya, Manqoba Mngqithi, kuelekea msimu wa 2026/27, klabu hiyo inatarajiwa kutangaza nyongeza nyingine katika benchi lake la ufundi kwa kumtambulisha raia wa Afrika Kusini, Yardaan Valodia, kama mchambuzi wa kiwango cha wachezaji (Performance Analyst).
Mngqithi ametua Yanga kuchukua nafasi ya Abdulhamid Moalin, ambaye alikuwa akiiongoza timu hiyo kwa muda baada ya mabadiliko ya benchi la ufundi.
Kwa mujibu wa taarifa zilizopatikana, Yanga na Valodia tayari wamekamilisha mazungumzo na kusaini mkataba, huku kilichobaki kikiwa ni tangazo rasmi kutoka kwa mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Valodia anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya benchi la ufundi la Mngqithi, akisimamia uchambuzi wa mechi, tathmini ya wachezaji na maandalizi ya mbinu za timu kabla na baada ya kila mchezo.
Ujio wake ni sehemu ya mkakati wa Yanga wa kuendelea kuimarisha idara ya ufundi kwa kuongeza wataalamu wenye uzoefu, ikiwa ni maandalizi ya kushindana kwa kiwango cha juu katika mashindano ya ndani na yale ya kimataifa msimu ujao.
Inatarajiwa Valodia aanze kazi mara moja sambamba na maandalizi ya kikosi hicho kuelekea msimu mpya, huku mashabiki wa Yanga wakisubiri kuona namna benchi jipya la ufundi litakavyoendeleza mafanikio ya klabu hiyo.