Yanga SC

Yanga Yatua Kwa Nduhumwe, Kanu Afichua Mpango Wa Singida

Vardo July 10, 2026 4:23 pm

BAADA ya Yanga kuonyesha nia ya kumsajili mshambuliaji wa Singida Black Stars, Amos Nduhumwe, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Muhibu Kanu, amesema kuondoka kwa nyota huyo hakutayumbisha mipango ya kikosi chake kuelekea msimu wa 2026/27.

Taarifa zinaeleza kuwa Yanga tayari imeanza hatua za kutafuta saini ya Nduhumwe, ambaye aling’ara msimu uliopita kwa kuonyesha kiwango bora na kuwa mmoja wa wafungaji muhimu wa Singida Black Stars.

Akizungumzia uwezekano wa mshambuliaji huyo kuhamia Yanga, Kanu amesema klabu yake haijawahi kutegemea mchezaji mmoja pekee, akisisitiza kuwa imekuwa na uwezo wa kuziba nafasi za nyota wanaoondoka bila kuyumba.

“Kwenda Yanga kwa Amos hakuathiri Singida. Msimu uliopita tulimpoteza Jonathan Sowah, lakini tuliingia sokoni na tukampata Amos ambaye alifanya vizuri. Hatuwezi kutegemea mchezaji mmoja,” amesema Kanu.

Ameongeza kuwa iwapo Nduhumwe ataondoka, Singida Black Stars itatumia nafasi hiyo kuingia sokoni kutafuta mbadala mwenye ubora wa kuendeleza ushindani ndani ya kikosi.

Kanu amesisitiza kuwa falsafa ya klabu hiyo ni kuendelea kuijenga timu yenye ushindani bila kujali mabadiliko ya wachezaji, akieleza kuwa uongozi unaendelea kufanya maandalizi ya kuhakikisha kikosi kinakuwa imara kwa ajili ya msimu wa 2026/27.

Spain dhidi ya Belgium, Vita ya Kisasi Lionel Messi, Kylian Mbappe Kama Pacha