Cecafa Cup

Droo Yawagonganisha Simba Na Singida Kagame Cup

Vardo July 10, 2026 3:55 pm

DROO ya hatua ya makundi ya michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026 imezikutanisha vigogo wa Tanzania, Simba SC na Singida Black Stars, ambao wamepangwa pamoja katika Kundi B. Mbali na timu hizo mbili, kundi hilo pia linaundwa na Jamus FC ya Sudan Kusini na MCC ya Somalia.

Kupangwa kwa Simba na Singida Black Stars katika kundi moja kunamaanisha mashabiki watashuhudia pambano la mapema la timu za Tanzania, huku kila upande ukisaka kumaliza kileleni mwa kundi ili kujihakikishia tiketi ya moja kwa moja ya kutinga hatua ya nusu fainali.

Kundi A linajumuisha mabingwa wa Rwanda, APR FC, Vipers SC ya Uganda, Gor Mahia ya Kenya na Garde Républicaine ya Djibouti. Hili linatajwa kuwa moja ya makundi yenye ushindani mkubwa kutokana na ubora na historia ya timu hizo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Kwa upande wa Kundi C, Al Hilal ya Sudan itaongoza vita dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda, Tusker FC ya Kenya na KVZ FC ya Zanzibar, katika kundi linalotarajiwa kushuhudia ushindani mkali wa kuwania nafasi ya kufuzu.

Kwa mujibu wa mfumo wa mashindano, timu itakayomaliza katika nafasi ya kwanza kwenye kila kundi itafuzu moja kwa moja hatua ya nusu fainali. Nafasi ya nne itachukuliwa na timu itakayokuwa na rekodi bora zaidi kati ya zile zitakazomaliza nafasi ya pili katika makundi yote matatu.

Michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026 unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya maandalizi ya msimu wa 2026/27 kwa klabu nyingi za ukanda huu. Kwa Simba na Singida Black Stars, mashindano hayo yatakuwa jukwaa la kupima ubora wa vikosi vyao na kuongeza makali kabla ya kuanza kwa mashindano rasmi ya msimu mpya.

Hakuna Pre-Season Ya Nje! Simba Yaweka Dau Kagame Spain dhidi ya Belgium, Vita ya Kisasi