Simba SC

Hakuna Pre-Season Ya Nje! Simba Yaweka Dau Kagame

Vardo July 10, 2026 3:42 pm

KLABU ya Simba imebadili mkakati wa maandalizi ya msimu wa 2026/27 kwa kuamua kutofanya kambi maalumu ya maandalizi (pre-season) nje ya nchi, badala yake ikipeleka nguvu zake katika ushiriki wa michuano ya Kombe la Kagame (CECAFA Kagame Cup).

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na klabu hiyo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, kikosi cha Simba kinatarajiwa kusafiri kuelekea Kigali, Rwanda, kushiriki michuano hiyo itakayofanyika kuanzia Julai 24 hadi Agosti 7, 2026.

Uamuzi huo unaelezwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa benchi la ufundi wa kuhakikisha wachezaji wapya wanaingia haraka katika mfumo wa timu, huku ushindani wa ndani ukijengwa kupitia mechi za mashindano badala ya kutegemea michezo ya kirafiki ya maandalizi.

Kupitia Kombe la Kagame, Simba itapata fursa ya kujipima dhidi ya baadhi ya klabu bora kutoka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Benchi la ufundi linatarajiwa kutumia michuano hiyo kutathmini uwezo wa kikosi, kuangalia mchanganyiko wa wachezaji na kubaini maeneo yanayohitaji maboresho kabla ya kuanza kwa mashindano rasmi ya msimu.

Baada ya kumaliza ushiriki wake nchini Rwanda, Simba itarejea Tanzania kwa ajili ya maandalizi ya mwisho ya mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga, utakaochezwa Agosti 12, 2026.

Mchezo huo unatarajiwa kuwa kipimo muhimu kwa Wekundu wa Msimbazi kabla ya kuanza rasmi kwa msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, unaotarajiwa kufunguliwa Agosti 14, 2026.

Barker Aizidi Kete Yanga Kwa Makgalwa Droo Yawagonganisha Simba Na Singida Kagame Cup