Simba SC

Simba Yafanya Uamuzi Wa Chasambi, Mkopo Waja Baada Ya Ushindani Mkali

Vardo July 13, 2026 10:56 am

NYOTA wa Simba,Ladaki Chasambi yupo kwenye hatua za kuondoka Simba kwa mkopo kuelekea msimu wa 2026/27, huku Mashujaa FC na Pamba Jiji zikitajwa kuwa vinara katika mbio za kuwania huduma yake.

Hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa Simba wa kumpa kiungo huyo nafasi ya kucheza mara kwa mara, baada ya kushindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza kutokana na ushindani mkubwa uliopo eneo la kiungo.

Chasambi alijiunga na Wekundu wa Msimbazi Januari 8, 2024, akitokea Mtibwa Sugar kwa mkataba wa miaka mitatu unaotarajiwa kumalizika Desemba 2026. Kutokana na mkataba wake kuendelea, uhamisho unaotarajiwa katika dirisha hili ni wa mkopo.

Awali kulikuwa na mpango wa kumrejesha Mtibwa Sugar kwa mkopo ili apate muda zaidi wa kucheza. Hata hivyo, baada ya klabu hiyo kushuka daraja, Mashujaa FC na Pamba Jiji zimejitokeza na kuonyesha nia ya kumsajili kwa mkopo.

Kwa mujibu wa chanzo cha karibu na mchezaji huyo, mazungumzo kati ya pande husika yanaendelea vizuri, huku uamuzi wa mwisho ukitarajiwa kufikiwa kabla ya Simba kukamilisha maandalizi yake ya msimu mpya.

Tangu kuwasili kwa kocha Steve Barker, Chasambi amekutana na ushindani mkali katika nafasi ya kiungo, akipambana na wachezaji kama Libasse Gueye, Elie Mpanzu na Inno Loemba ambao wamekuwa wakipewa nafasi zaidi kutokana na viwango vyao.

Msimu uliopita chini ya kocha Fadlu Davids, Chasambi alitumika katika nafasi mbalimbali, ikiwemo beki wa kushoto, lakini bado hakufanikiwa kujenga nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Kutokana na hali hiyo, Simba inaamini kumpeleka kwa mkopo kutampa nafasi ya kucheza mara kwa mara, kuongeza kiwango chake na kurejea Msimbazi akiwa na uzoefu zaidi wa ushindani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Kiungo Wa Nigeria Akaribia Msimbazi, Simba Yapiga Hesabu Kubwa Messi Ana Jambo Lake Kwa England