England vs Argentina: FBI yaipa mechi hadhi ya hatari kubwa zaidi Kombe la Dunia 2026
ATLANTA, MAREKANI: POLISI nchini Marekani wameweka tahadhari ya kiwango cha juu kuelekea mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia 2026 kati ya England na Argentina utakaochezwa Jumatano kwenye Uwanja wa Mercedes-Benz mjini Atlanta, kufuatia hofu ya kutokea kwa vurugu kati ya mashabiki wa mataifa hayo mawili.
Katika maandalizi ya kuhakikisha usalama unaimarishwa, FBI, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), pamoja na vyombo vya usalama vya eneo la Atlanta walifanya kikao maalumu Jumatatu kujadili hatua za kudhibiti hali hiyo.
Tatizo hilo limetokana na mfumo wa mauzo ya tiketi wa FIFA, ambapo tiketi zilizonunuliwa kupitia vyama vya soka vya England na Argentina zimepangiwa maeneo maalumu ya kukaa, lakini tiketi zilizouzwa moja kwa moja na FIFA zinawaruhusu mashabiki wa timu zote mbili kukaa katika maeneo yanayofanana.
Maofisa wa usalama wanatarajia uwanja kugawanyika karibu sawa kati ya mashabiki wa England na Argentina, huku kila upande ukitarajiwa kuwa na maelfu ya wafuasi waliowasili kutoka mataifa yao pamoja na raia wanaoishi Marekani.
Historia ya ushindani kati ya mataifa hayo imekuwa moja ya sababu kuu zilizofanya mchezo huo kupewa hadhi ya “hatari kubwa”.
Mbali na kumbukumbu ya robo fainali ya Kombe la Dunia mwaka 1986, ambapo Diego Maradona aliifungia Argentina bao maarufu la “Mkono wa Mungu” dhidi ya England, pia kuna kumbukumbu za vita vya visiwa vya Falkland mwaka 1982 vilivyozikutanisha nchi hizo mbili na kusababisha vifo vya watu 907 kabla ya Uingereza kurejesha udhibiti wa visiwa hivyo.
Mvutano huo uliibuka tena baada ya ushindi wa Argentina dhidi ya Uswisi katika robo fainali, ambapo baadhi ya wachezaji walionekana kuimba nyimbo zinazorejelea suala la Falkland. Wiki hii pia Waziri wa Mambo ya Nje wa Argentina alisisitiza tena madai ya nchi yake juu ya visiwa hivyo, madai yaliyokataliwa mara moja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer.