Burudani

Abdalla Hemba: Nilikata Tamaa, Sasa Nimepona, Nipo Tayari Kurudi Jukwaani

Vardo July 15, 2026 10:33 am

BAADA ya miezi kadhaa ya kupambana na maradhi yaliyomweka mbali na muziki, msanii wa Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukaye’, Abdalla Hemba amefunguka kuhusu safari yake ya ugonjwa, namna alivyopoteza fahamu, watu aliowakuta wamemtafuta kupitia simu yake na matumaini yake ya kurejea jukwaani.

Dakika 5 Na… ilimtafuta na kuzungumza naye kuhusu maendeleo yake kiafya na amefunguka mengi ikiwamo hamu yake ya kurejea jukwaani na aliyoyapitia kipindi anaumwa, familia yake ilivyopambana naye pamoja na marafiki waliokuwa karibu naye.

Hemba: Namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kupata afya njema. Kwa sasa naendelea vizuri na ninajisikia mwenye nguvu tofauti na nilivyokuwa awali. Baada ya yote niliyopitia, ninaamini Mungu amenipa nafasi nyingine ya maisha.

Hemba: Kilikuwa kipindi kigumu sana. Ukweli nilifikia hatua nikajikatia tamaa ya kuishi. Lakini kuumwa ni jambo la ibada, hakuna anayeweza kulikwepa. Leo namshukuru Mungu kwa kunivusha salama.

Hemba: Hapana. Kuna kipindi sikuwa natambua chochote. Sikuwatambua watu waliokuwa karibu yangu wala waliokuwa wananitembelea. Hata simu sikuwa na uwezo wa kuitumia.

Hemba: Nilishangaa sana. Nilipoanza kupata nafuu nikachukua simu yangu ndipo nikaanza kuona simu nyingi za watu waliokuwa wamenitafuta pamoja na ujumbe walionitumia. Nilikaa nikipitia mmoja baada ya mwingine kuona nani alinipigia na kunitumia salamu za kunifariji. Niliguswa sana.

Hemba: Nawashukuru sana. Wadau, marafiki, mashabiki na kila aliyesimama nami wakati wa ugonjwa wangu, Mungu awabariki. Sapoti yao imenipa nguvu kubwa ya kuendelea kupambana.

Hemba: Familia yangu imekuwa nguzo kubwa sana. Wamenihudumia na kunipa moyo katika kila hatua ya matibabu. Bila wao na msaada wa Mungu isingekuwa rahisi kufika hapa nilipo leo. Pia walikuwa wanawapokea wageni wangu vizuri sana hivyo kila aliyekuja kuniona wameniambia na kila kilichokuwa kinaendela wameniambia.

Hemba: Kwa sasa nipo vizuri na ninaendelea kuimarika kila siku. Nipo tayari kurudi jukwaani kuwaburudisha mashabiki wangu. Muziki ndiyo maisha yangu na nimeumisi sana kuutazama nikiwa pembeni.

Hemba: Waendelee kuniombea. Nawashukuru kwa upendo wao, simu zao, ujumbe wao na dua walizoniombea. Upendo wao ndiyo uliokuwa unanipa matumaini hata wakati ambao sikuwa na uwezo wa kuzungumza.
Historia ya kuugua

Hemba alianza kuugua Machi 22, 2026 baada ya kupimwa na kugundulika ana malaria na UTI. Awali alilazwa Hospitali ya Malawi iliyopo Kiwalani kabla ya hali yake kuzidi kuwa mbaya na kuhamishiwa Hospitali ya Temeke kwa matibabu zaidi.

Baadaye madaktari walibaini pia alikuwa na changamoto nyingine za kiafya zikiwemo kisukari, shinikizo la damu (BP), nimonia na kifua kikuu (TB), hali iliyomfanya kupoteza nguvu, kushindwa kutembea kwa muda na kupata matatizo ya kula. Katika mahojiano yake ya awali na Mwanaspoti alisema alikuwa akihudhuria kliniki kila Jumanne huku akiendelea na matibabu na uangalizi wa karibu.

Sasa, baada ya miezi kadhaa ya matibabu, Hemba amesema afya yake imeimarika, amerejea katika hali nzuri na yupo tayari kurudi jukwaani kuendelea na kazi yake ya kuwaburudisha mashabiki wa muziki wa dansi.

O’reilly:  Nafurahi Kumkabili Messi