Simba Yatoa Ruhusa Kwa Bajaber, Safari Ya Timu Mpya Yaanza
UONGOZI wa klabu ya Simba SC umefikia makubaliano na kiungo wake, Bajaber, kuhusu hatua inayofuata ya maisha yake ya soka, huku akiruhusiwa kuendelea kuwa sehemu ya kikosi kwa muda wakati akisubiri kupata klabu mpya.
Katika mazungumzo yaliyofanyika kati ya pande hizo mbili, Bajaber aliwasilisha ombi maalum kwa viongozi wa Simba SC la kuendelea kubaki na timu hiyo kwa kipindi cha mpito, huku akiendelea na mchakato wa kutafuta changamoto mpya nje ya klabu.
Taarifa zinaeleza kuwa uongozi wa Simba SC umelikubali ombi hilo na kumpa nafasi kiungo huyo kuendelea kuungana na kikosi katika maandalizi ya msimu mpya wa 2026/27, endapo atakuwa hajafanikiwa kupata timu nyingine kabla ya kuanza kwa kambi ya pre-season.
Hatua hiyo inampa Bajaber nafasi ya kusafiri na kikosi cha Simba kwenda kambini na kushiriki baadhi ya programu za maandalizi, ingawa akiwa katika kipindi cha kusubiri uamuzi wa mwisho kuhusu hatma yake ya kisoka.
Hata hivyo, uwepo wake ndani ya kikosi hicho hautakuwa sehemu ya mipango ya muda mrefu ya Simba SC kwa msimu ujao, huku mabingwa hao wa Kombe la Muungano na CRDB Federation Cup wakiendelea na mikakati ya kukiimarisha kikosi kwa ajili ya mashindano ya ndani na ya kimataifa.
Kwa sasa, pande zote mbili zimeendelea kuheshimiana katika mchakato huo, huku Bajaber akipewa muda wa kutafuta sehemu mpya ya kuendeleza safari yake ya soka na Simba ikiendelea na maandalizi ya msimu mpya wenye malengo makubwa.