Simba SC

Simba Yatuma Ujumbe Mzito, Usajili Mpya Wakitisha Ligi Na CAF

Vardo July 15, 2026 2:35 pm

UONGOZI wa klabu ya Simba umeweka wazi dhamira yake kuelekea msimu wa 2026/27, ukisisitiza kuwa haitaki kuridhika na mafanikio ya msimu uliopita bali inalenga kurejea kwa nguvu kwenye mbio za mataji ya ndani na kufanya vizuri zaidi kwenye michuano ya kimataifa.

Simba imefanikiwa kutwaa taji moja msimu uliopita, lakini sasa imeweka nguvu kubwa katika kuimarisha kikosi chake kwa lengo la kuhakikisha inakuwa na uwezo wa kushindania mataji mengi zaidi msimu unaokuja.

Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema mafanikio yaliyopatikana yamekuwa chachu ya kuongeza kasi ya maandalizi kuelekea msimu mpya, huku usajili unaofanywa ukiwa sehemu ya mpango wa kujenga kikosi chenye ushindani mkubwa.

“Baada ya kutwaa taji moja msimu uliopita sasa tunawekeza nguvu kwenye msimu unaokuja kuhakikisha tunapata mataji mengine. Hilo ndilo jambo kubwa tunalolenga,” amesema Ahmed.

Amesema msimu wa 2026/27 hautakuwa wa majaribio kwa Simba, kwani matarajio ya mashabiki wa klabu hiyo ni kuona timu ikirejea kileleni mwa Ligi Kuu Tanzania Bara na kuonyesha makali yake kwenye mashindano ya kimataifa.

“Msimu unaokuja hakutakuwa na dharura yoyote, Wanasimba wanataka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara na wanataka kumuona Simba akirejea kwa nguvu katika michuano ya kimataifa,” amesema.

Ahmed ameongeza kuwa aina ya usajili unaofanywa na klabu hiyo ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha Simba inakuwa na kikosi imara kitakachoweza kupambana kwenye kila jukwaa, kuanzia ligi ya ndani hadi mashindano ya Afrika.

“Kwa aina ya usajili tunaoufanya msimu huu tunaona kuna mwanya mkubwa wa Simba kufanya vizuri katika Ligi na michuano ya kimataifa. Hayo ndiyo malengo yetu makubwa msimu ujao,” ameongeza.

Simba imeendelea kufanya maboresho katika kikosi chake kuelekea msimu mpya, huku uongozi ukisisitiza kuwa lengo kuu ni kurejesha heshima ya klabu hiyo kwa kutwaa mataji zaidi na kuwa na ushindani mkubwa ndani na nje ya Tanzania.

Pacome Kutimkia Paris Yanga Waeleza Haya… England Na Argentina Wapambana Kwa Nafasi Ya Fainali