Pacome Kutimkia Paris Yanga Waeleza Haya…
KIUNGO wa Yanga, Pacome Zouzoua, ametoka hospitalini na kwa sasa anaendelea na hatua za awali za kupona akiwa nyumbani, huku akijiandaa kusafiri kwenda Paris, Ufaransa, kwa ajili ya matibabu na uangalizi zaidi wa jeraha alilopata.
Pacome alipata jeraha hilo katika mchezo wa mwisho wa msimu uliopita dhidi ya JKT Tanzania, hali iliyomfanya kufanyiwa upasuaji na kuanza mchakato wa kurejea uwanjani.
Msemaji wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Ali Kamwe, amesema safari ya kwenda Paris imelenga kuhakikisha kiungo huyo anapata uangalizi maalumu ili kurejea akiwa katika kiwango bora na tayari kwa soka la ushindani.
“Baada ya kufanyiwa upasuaji, tunasubiri zipite zile wiki sita ambazo daktari alitoa kama sehemu ya uangalizi wa jeraha lake. Baada ya hapo tutapata makadirio ya muda ambao atakuwa nje ya uwanja,” amesema Kamwe.
Ameongeza kuwa kwa sasa Pacome ameshatoka hospitalini na yupo nyumbani akijiandaa na safari hiyo ya matibabu, huku hatua zote zikichukuliwa kwa umakini kutokana na ukubwa wa jeraha alilolipata.
Wakati huo huo, Kamwe ametoa taarifa kuhusu hali za wachezaji wengine waliokuwa majeruhi ndani ya kikosi hicho, akiwemo kipa namba tatu, Khomen Abubakar, ambaye ameanza kuimarika na sasa yupo katika hatua za kurejea uwanjani.
“Khomen ameimarika kwa asilimia 85, ameshacheza mechi za hisani baada ya kuumia nyonga. Kinachofuata kwake ni kufanya mazoezi ya kuongeza nguvu (fitness) na kisha atarejea rasmi,” amesema.
Kuhusu mabeki Dickson Job na Clement Mzize, Kamwe amesema wawili hao wanaendelea na programu maalumu za matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na huenda wakarejea kwenye mechi za ushindani mwishoni mwa mwaka.
“Dickson Job na Clement Mzize wapo kwenye programu moja kwa mujibu wa ripoti za madaktari. Makadirio ni kuwa wanaweza kuonekana uwanjani katika mechi za ushindani wiki za mwisho za Novemba au mwanzoni mwa Desemba,” amesema Kamwe.