Bondia Roméo Katompa ‘Bololo’ Auawa Kwa Kuchomwa Moto Afrika Kusini
GAUTENG, AFRIKA KUSINI: Jamii ya michezo na raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wamegubikwa na majonzi mazito kufuatia ripoti za kusikitisha za kuuawa kwa bondia nyota, Roméo Katompa Kaboya, anayefahamika zaidi kama “Bololo”.
Katompa anadaiwa kuuawa kinyama kwa kuchomwa moto ndani ya nyumba yake iliyopo jimbo la Gauteng, Afrika Kusini, katika tukio linalohusishwa na wimbi jipya la chuki dhidi ya wageni (xenophobia).
Picha za kutisha zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaonyesha nyumba hiyo ikiteketea kabisa kuanzia ghorofa ya chini hadi juu. Mwili wa bondia huyo ulipatikana ndani ya chumba cha kulala ukiwa umeungua vibaya sana kifudifudi, kiasi cha kutambulika kwa shida.
Wasifu na Historia Yake ya Ulingoni
Katompa, mzaliwa wa Mbuji-Mayi nchini DRC, alikuwa akiishi Afrika Kusini ambako alimuoa mwanamke mzawa na kufanikiwa kupata naye mtoto mmoja. Mbali na mapambano yake binafsi, alikuwa akifahamika pia kama mshirika wa karibu wa mazoezi (sparring partner) wa bondia nguli wa dunia, Junior Makabu.
Katika ngumi za kulipwa ambazo alizianza rasmi Julai 20, 2018, Katompa (anayepigana staili ya orthodox) alishiriki mapambano sita; alishinda manne yote kwa KO na kupoteza mawili kwa KO. Pambano lake la mwisho lilikuwa Novemba 8, 2025, mjini Kigali, Rwanda, ambapo alipoteza dhidi ya Tamba Merlin.
Hofu na Sintofahamu Yatawala
Kifo chake kimeamsha upya hofu kubwa kuhusu usalama wa wahamiaji nchini Afrika Kusini, huku baadhi ya wachambuzi wakilalamikia ukimya wa mamlaka za nchi hiyo dhidi ya matendo ya ukatili wa xenophobia. Hadi sasa, jeshi la polisi na mamlaka za Afrika Kusini bado hazijatoa taarifa rasmi kuthibitisha au kukanusha tukio hilo.