Seth Curry Golden State Warriors
Habari za michezo

Seth Curry Afunguka Mustakabali Wake Golden State Warriors

Vardo July 18, 2026 3:23 pm

SAN FRANCISCO, MAREKANI – Nyota wa mpira wa kikapu, Seth Curry, ameweka wazi kuwa yuko tayari kuongeza mkataba na kuendelea kuitumikia klabu ya Golden State Warriors, mradi tu pande zote mbili zifikie makubaliano katika kipindi hiki cha usajili wa wachezaji huru (free agency).

Seth, ambaye ni mdogo wake na nguli wa Warriors, Stephen Curry, alikiri kuwa msimu uliopita ulikuwa mgumu sana kwake kutokana na changamoto za majeraha zilizomfanya kucheza mechi 10 pekee. Pamoja na changamoto hizo, amesisitiza kuwa bado ana mapenzi makubwa na timu hiyo.

Akizungumza wakati wa mashindano ya gofu ya American Century Championship yaliyofanyika South Lake Tahoe, Curry alieleza kuwa kipaumbele chake kikubwa kwa sasa ni kurudisha utimamu wa mwili wake kwa asilimia 100 kabla ya kufanya uamuzi wa hatua inayofuata.

“Ninachofanya sasa ni kujaribu kuwa fiti kabisa, kisha nione kitakachotokea Julai na Agosti kwenye soko la wachezaji huru. Kuna mabadiliko mengi yanayoendelea kwenye ligi, kwa hiyo ninatafuta mazingira bora zaidi kwangu,” alisema Curry.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 35 alisaini mkataba wa mwaka mmoja na Warriors mnamo Desemba mwaka jana. Hata hivyo, kutokana na majeraha yaliyomkabili yeye na kaka yake Steph, wawili hao walifanikiwa kucheza pamoja mechi tatu tu za msimu wa kawaida.

Alipoulizwa kama angependa kurejea Warriors, Seth alijibu bila kusita: “Bila shaka. Sikupata fursa ya kuonyesha kila nilichotaka uwanjani msimu uliopita, lakini nina heshima kubwa sana kwa klabu hii na mashabiki wake. Ni sehemu yenye mazingira ya kiwango cha juu mno.”

Licha ya kukabiliwa na majeraha na kucheza mechi chache, Seth alionyesha cheche zake kama mmoja wa wafungaji bora wa mashuti ya mbali. Katika mchezo wake wa kwanza msimu uliopita, alifunga pointi 14 kwa usahihi mkubwa, akihitimisha msimu kwa kufunga mashuti 12 kati ya 25 ya alama tatu (3-pointers).

Akiwa kama mchezaji huru kwa sasa, mustakabali wake uwanjani unatazamwa kwa ukaribu. Hata hivyo, amebainisha kuwa hafikirii sana kuhusu kustaafu, bali anachukua maamuzi msimu hadi msimu.

“Nimecheza NBA kwa miaka 13 sasa. Nilipoingia kwenye ligi hii bila hata kuchaguliwa kwenye Draft, ndoto yangu ilikuwa kucheza angalau miaka 10 na nililazimika kupambana kwa kila hatua. Sijaridhika bado, lakini ninajivunia nilichofikia. Kwa sasa nitaangalia msimu mmoja baada ya mwingine, hasa unapopitia majeraha kama haya,” alihitimisha Curry.

Warriors sasa wako kwenye mtihani wa kuamua kama watampa mkataba mpya mkali huyo wa mashuti ya mbali kabla ya msimu mpya wa NBA kuanza.

Nani Unampa Nafasi Ya Kukupatia Ushindi Leo?