Yanga SC Kutangaza Wachezaji Kimataifa: Ali Kamwe Afunguka Usajili
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wameonyesha nia ya dhati ya kuendeleza utawala wao nchini na barani Afrika kuelekea msimu mpya wa 2026/27, baada ya kukamilisha awamu ya kwanza ya usajili wa wachezaji wazawa na sasa kugeukia ‘shoti za kimataifa’.
Afisa Habari na Mawasiliano wa Yanga SC, Ali Kamwe, ameeleza kuwa usajili uliofanywa msimu huu umeandaa kikosi imara chenye ushindani mkubwa katika kila nafasi, chenye uwezo wa kutetea mataji ya ndani na kufika mbali zaidi kwenye michuano ya kimataifa.
Mwijage Akamilisha Orodha ya Wazawa
Kamwe amethibitisha kuwa klabu hiyo imehitimisha rasmi zoezi la kuwatambulisha wachezaji wa ndani, ambapo nyota wa mwisho kutambulishwa alikuwa beki wa kati, Eric Mwijage, aliyesajiliwa akitokea KMC FC.
“Tulianza kwa kuwatangaza wachezaji wazawa na tuna imani kubwa kuwa wana uwezo na viwango vya kubeba matarajio makubwa ya Wanayanga. Kuanzia hivi sasa, tunaingia hatua inayofuata ya kutangaza majina ya wachezaji wa kigeni,” alisema Ali Kamwe.
Kuzingatia Ubora na Mahitaji ya Benchi la Ufundi
Uongozi wa Wananchi umesisitiza kuwa mchakato wa usajili msimu huu haukufanywa kwa kufuata mikumbo, bali umezingatia kwa umakini mkubwa mahitaji halisi ya benchi la ufundi na viwango vya juu vya wachezaji waliosajiliwa.
Lengo kuu la Yanga SC si kutawala tu soka la nyumbani (NBC Premier League), bali pia kuunda kikosi tishio kitakachotikisa na kushindana vikali na miamba ya soka barani Afrika katika msimu wa 2026/27. Mashabiki wametakiwa kukaa tayari kupokea taarifa za nyota hao wa kimataifa mmoja baada ya mwingine.