Mabondia wa Tanzania Waanza Kusaka Medali Glasgow!
Timu ya Taifa ya ngumi ya ridhaa ya Tanzania leo imeanza rasmi safari ya kusaka medali na heshima katika Michezo ya Jumuiya ya Madola 2026 inayotimua vumbi jijini Glasgow, Uskoti. Mabondia watatu wa Kitanzania wanatarajiwa kuingia ulingoni katika ukumbi maarufu wa Scottish Event Campus (SEC).
Ratiba ya droo rasmi imeiweka Tanzania kwenye mtihani mzito wa mapema, ikikutana na wapinzani wakali kutoka Nigeria, Zambia na Lesotho. Mashindano haya makubwa yatakayorindima mpaka Agosti 1, 2026, yanashirikisha jumla ya mabondia 201 (wanaume 131 na wanawake 70) kutoka mataifa 43 ya Jumuiya ya Madola.
Vita ya Ulingoni: Nani Anapambana na Nani?
-
Yusuf Changalawe (Uzani wa Light Heavyweight – Kilo 80): Mkali huyu anayeongoza jahazi la Tanzania ataonyeshana kazi na Ankintola David kutoka Nigeria katika hatua ya raundi ya 32.
-
Faki Issa Faki (Uzani wa Bantamweight – Kilo 55): Ataanza msako wake wa medali kwa kupambana na Mwengo Mwale wa Zambia, pia katika hatua ya raundi ya 32.
Zawadi Kutaka “Malkia wa Tanzanite” Kuandika Historia!
Matumaini makubwa ya Tanzania kupata medali ya mapema yameelekezwa kwa Zawadi Kutaka, maarufu kama “Malkia wa Tanzanite”.
Bondia huyu anayepigana katika uzani wa featherweight (kilo 57) tayari ameingia kwenye vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mwanamke wa kwanza kabisa kutoka Tanzania kuiwakilisha nchi katika mchezo wa ngumi kwenye Michezo ya Jumuiya ya Madola.
Kwa bahati nzuri, Kutaka amefuzu moja kwa moja (bye) hadi hatua ya robo fainali, hivyo anahitaji ushindi wa pambano moja pekee dhidi ya bondia kutoka Lesotho ili kujihakikishia medali.
Wawakilishi Wengine wa Tanzania Glasgow 2026
Mbali na mchezo wa ngumi, Tanzania imetuma wawakilishi katika michezo mingine mitatu:
-
Riadha: Wanariadha 6 watashuka kwenye Uwanja wa Scotstoun kuanzia Jumatatu, Julai 27.
-
Judo: Wachezaji 2 watatoana sweat ukumbi wa SEC kuanzia Julai 31 hadi Agosti 2.
-
Kuogelea: Collins Saliboko anaanza kutoa mawimbi leo katika bwawa la Tollcross International Swimming Centre.