Kagera Sugar usajili wa Mudathir Said
Michezo Bongo

Kagera Sugar Yakamilisha Usajili wa Mudathir Said, Yanasa Nyota Wengine Kibao!

Vardo August 5, 2026 9:08 am

KAGERA: Baada ya kufanikisha lengo la kurejea na kukata tiketi ya kucheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa 2026-2027, uongozi wa Kagera Sugar umeanza kusuka upya kikosi chao kwa ajili ya kuleta ushindani wa kweli.

Mabosi wa klabu hiyo wapo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa aliyekuwa kiungo/mshambuliaji wa Mashujaa FC, Mudathir Said, ambaye amesaini mkataba wa miaka miwili kuwatumikia matajiri hao wa sukari.

Mudathir, aliyejiunga na Mashujaa FC Julai 29, 2025 akitokea Mbeya City, ameamua kuvunja mkataba wake wa mwaka mmoja uliokuwa umebaki ili kutua Kagera Sugar baada ya kuwekewa mezani dau nono lililomshawishi. Nyota huyo pia anakumbukwa kwa mchango wake akiwa na timu za Coastal Union na Pamba Jiji.

Akizungumza na mtandao wa Soka la Bongo, Meneja wa Kagera Sugar, Bernard Samson Sikira, amethibitisha kuwa usajili wa kikosi kipya umekamilika kulingana na matakwa ya benchi la ufundi.

“Tumebakisha baadhi ya taratibu ndogo kabla ya kuweka wazi kikosi chetu cha msimu wa 2026-2027. Usajili wetu umezingatia kwa kina mapendekezo ya benchi la ufundi na malengo tuliyojiwekea ya kufanya vizuri na kuleta ushindani wa hali ya juu Ligi Kuu,” alisema Sikira.

Majina Mipya Yaliyotua Kagera Sugar: Mbali na Mudathir Said, Kagera Sugar imefanya uwekezaji mkubwa kwa kuleta wachezaji wengine wa kimataifa na wa ndani:

  • Boniface Onyango: Beki wa kushoto anayemudu pia kucheza beki ya kati kutoka Kakamega Homeboyz (Kenya).

  • Collins Maina: Mshambuliaji hatari kutoka Fortune Sacco FC (Kenya).

  • Naku James: Mshambuliaji aliyesajiliwa kutoka Polisi Tanzania.

  • Said Ndemla: Kiungo mzoefu aliyetokea JKT Tanzania.

  • Daudi Milandu: Kiungo mshambuliaji kutoka Dodoma Jiji.

  • Dickson Mhilu: Beki wa kulia anayerejea klabuni hapo akitokea Dodoma Jiji.

Ujio wa nyota hawa wapya unadhihirisha dhumuni la Kagera Sugar sio tu kushiriki Ligi Kuu, bali kupambana na kurejesha heshima yao katika soka la Bongo.

Deogratius Mafie Aingia Makubaliano na Pamba Jiji, Aaga Kagera Sugar Twiga Stars Yaaga WAFCON 2026 Kwa Kipigo Cha Ivory Coast