Deogratius Mafie Pamba Jiji
Michezo Bongo

Deogratius Mafie Aingia Makubaliano na Pamba Jiji, Aaga Kagera Sugar

Vardo August 5, 2026 9:00 am

Klabu ya Pamba Jiji ipo katika hatua za mwisho kabisa kukamilisha usajili wa mshambuliaji hatari, Deogratius Mafie, kufuatia uamuzi wake wa kuachana na kikosi cha Kagera Sugar alichokisaidia kupanda Ligi Kuu Bara kwa msimu wa 2025-2026.

Akizungumza na mtandao huu wa Soka la Bongo, Mafie amethibitisha kuwa mkataba wake na Kagera Sugar umefikia kikomo baada ya kumalizika kwa msimu na sasa yupo tayari kuanza changamoto mpya sehemu nyingine.

“Ni kweli nimefikia uamuzi wa kuondoka na nipo tayari kwa ajili ya kutafuta changamoto mpya. Mazungumzo ya kuongeza mkataba mwingine wa kuichezea Kagera Sugar yalikuwepo, lakini nimeona huu ni muda sahihi wa kwenda sehemu nyingine,” alisema Mafie.

Licha ya kauli hiyo ya mchezaji, taarifa za ndani zinathibitisha kuwa nyota huyo—ambaye pia aliwahi kucheza Biashara United—yupo hatua za mwisho kujiunga na miamba hiyo ya Mwanza baada ya pande zote mbili kufikia makubaliano mazuri.

Akiweka sawa suala la usajili ndani ya klabu hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji, Ezekiel Ntibikeha, ameeleza kuwa usajili wao kwa msimu mpya wa 2026-2027 umekamilika kwa kiasi kikubwa na kilichobaki ni idara ya habari kuwatambulisha wachezaji hao rasmi.

Mafie anatarajiwa kuungana na nyota wengine wapya waliotua Pamba Jiji kuboresha kikosi hicho, akiwemo kipa Steve Ochieng (Shabana FC – Kenya), Erick Johola (Mashujaa FC), Nonyem Okorocha (Mlandege FC), Frank Ernest (KMC FC), na Ally Saleh Machupa ‘Machupa Jr’ (Namungo FC).

Wengine waliokamilisha usajili ni Salehe Karabaka (Simba SC), Fadhili Baluba (Raskazone FC), John Ochieng (Zanaco FC), beki wa kulia Abdallah Said Ali ‘Lanso’, pamoja na mshambuliaji raia wa DR Congo, Malanga Horso Mwaku kutokea Singida Black Stars anayejiunga kwa mkopo wa msimu mmoja.

Rayon Sports Yaitinga Fainali CECAFA Kagame Cup 2026 baada ya Kuichapa Jamus SC Kagera Sugar Yakamilisha Usajili wa Mudathir Said, Yanasa Nyota Wengine Kibao!