Clara Luvanga: Kuvunja Rekodi ya Dunia ni Mtihani Mkubwa Washington Spirit
Mshambuliaji mpya wa klabu ya Washington Spirit nchini Marekani, Mtanzania Clara Luvanga, ameweka wazi kuwa usajili wake uliovunja rekodi ya dunia katika soka la wanawake ni jambo linalompa faraja kubwa, lakini pia unaleta mtihani mzito katika career yake.
Clara ameweka historia hiyo baada ya kukamilisha usajili wa kitita cha Dola milioni 2.3 kutoka Al Nassr ya Saudi Arabia kwenda Washington Spirit, na kumfanya kuwa mchezaji ghali zaidi kwenye historia ya soka la wanawake barani Ulaya na duniani kote.
“Namba Hizi Zinakuja na Wajibu Mkubwa”
Akizungumzia usajili huo, Clara ameeleza kuwa ingawa anafurahia thamani kubwa aliyowekewa, anatambua vyema kuwa thamani hiyo inahitaji majibu ya vitendo ndani ya uwanja.
“Najisikia furaha kuwa mchezaji wa thamani zaidi, lakini kuna ugumu unaokuja nyuma yake. Ni rahisi kufurahia namba za fedha zilizowekwa, lakini unapaswa kukumbuka kuna wachezaji wakubwa wapo Chelsea, Bayern Munich, Real Madrid, na Barcelona,” amesema Clara.
Ameongeza kuwa malengo yake kuu sasa ni kudhibitisha ubora wake ili kuendana na thamani hiyo:
“Hizo namba zilikuja kwa sababu ya kile nilichokionesha awali. Sasa inapaswa nionyeshe zaidi ya wengine waliopo kwenye timu kubwa na maarufu duniani. Kwangu huu ni mtihani na lazima nipambane ili kuendelea kuonyesha thamani yangu.”
Kuanza kwa Malengo Mapya Washington Spirit
Mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga Princess ameeleza kuwa kwa sasa anazelekeza nguvu zake zote kwenye kituo chake kipya cha kazi ili kufanikisha malengo ya timu na zake binafsi.
-
Kuelewa Mfumo: Kuanza kwa kufahamu mahitaji ya kocha na mbinu za timu.
-
Msaada kwa Timu: Kuhakikisha anasaidia klabu kufikia malengo yake ya msimu.
-
Namba Binafsi: Kupambana kupata takwimu bora uwanjani kama mfungaji.
Ushauri Mzito kwa Wachezaji wa Kitanzania Nje ya Nchi
Pia, Clara hakusita kutoa neno la hamasa kwa wachezaji wenzake wa Kitanzania wanaopambana kucheza soka la kulipwa nje ya nchi, akiwataka kuwa wavumilivu dhidi ya changamoto za maisha ya ugenini.
Amezitaja changamoto kama upweke, tofauti za lugha, na kukaa mbali na familia kuwa ni vitu vya kawaida kwenye safari ya mafanikio, hivyo hawapaswi kukata tamaa na kurejea nyumbani mapema kabla ya kutimiza ndoto zao.