Jezi Mpya za Taifa Stars
Michezo Bongo

Waziri Makonda Asambaratisha Mchakato wa Jezi Mpya Taifa Stars, Auundia Tume Mkataba

Vardo September 18, 2026 3:02 pm

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imegomea rasmi na kutotambua matangazo ya jezi mpya za Timu za Taifa za Mpira wa Miguu (Taifa Stars), ikieleza kuwa mchakato wa kuzibadilisha haukuishirikisha Wizara licha ya maelekezo yaliyotolewa mapema mwezi Februari mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa leo, Septemba 18, 2026, imebainisha kuwa Waziri wa sekta hiyo, Paul Christian Makonda, hatambui utambulisho wa jezi hizo zilizotangazwa hivi karibuni na Naibu Waziri wake, Hamis Mohamed Mwinjuma ‘Mwana FA’.

Imeelezwa kuwa mwezi Februari 2026, Waziri Makonda alitoa maelekezo ya msingi kwamba, kwa kuwa Serikali inawekeza kiasi kikubwa cha fedha katika kuziandaa timu za taifa, kulikuwa na haja kubwa ya kuboresha jezi hizo ili ziakisi manufaa mapana ya kiuchumi na utambulisho wa nchi.

Suala la muonekano wa timu za taifa limepewa uzito mkubwa zaidi kwa sasa kutokana na Tanzania kujiandaa kuwa miongoni mwa nchi wenyeji wa Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Hatua za Kisheria na Uchunguzi wa Mkataba

Pamoja na kutotambua jezi hizo, Wizara imetangaza kuwa Waziri Makonda ataunda Kamati Maalum ya kuchunguza mkataba wa mzabuni wa jezi hizo. Lengo kuu ni kubaini manufaa ya kifedha yanayopatikana kwa timu za taifa, ambazo zimekuwa zikitumia fedha nyingi za walipa kodi huku fursa za mauzo ya jezi zikionekana kutochangia ipasavyo uendeshaji wa timu.

Kauli ya TFF na Mjadala Mtandaoni

Hatua hii ya Wizara imekuja kufuatia picha za jezi hizo kusambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii na kuibua maswali mengi kutoka kwa wadau wa soka kuhusu utaratibu na idhini iliyotumika.

Akizungumzia utata huo, Afisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Clifford Mario Ndimbo, alisema kuwa timu za taifa hazina changamoto ya mavazi na zinaendelea kutumia jezi zao za siku zote. Ndimbo aliongeza kuwa suala hilo linalojadiliwa mtandaoni kwa sasa linashughulikiwa na mamlaka za juu na TFF isingependa kuliingilia kwa undani.

Monza Kukutana na Sassuolo, Serie A Ikram Said: Uhamiaji FC Wapo Tayari Kutwaa Ubingwa Zanzibar