Rayon Sports Yaitinga Fainali CECAFA Kagame Cup 2026 baada ya Kuichapa Jamus SC
Miamba ya soka nchini Rwanda, Rayon Sports, inaendelea kuonyesha ubabe baada ya kufanikiwa kutinga fainali ya Kombe la CECAFA Kagame Cup 2026 kufuatia ushindi mnono wa mabao 3-1 dhidi ya Jamus SC ya Sudan Kusini katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa kwenye Uwanja wa Kigali Pele.
Ushindi huo umeifanya Rayon Sports kuendeleza rekodi yake ya kuvutia ya kushinda mechi zote (100%) tangu kuanza kwa mashindano hayo. Sasa miamba hiyo inajiandaa na pambano la kukata na shoka la fainali dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, mchezo utakaopigwa Agosti 7, 2026, kwenye Uwanja wa Amahoro.
Dk 90 za Burudani na Mabao
Rayon Sports, iliyomaliza kinara wa Kundi C kwa kushinda mechi zote za hatua ya makundi, ilianza mchezo kwa kasi na kupata bao la kuongoza mapema katika dakika ya 17 kupitia kwa kiungo wa kimataifa wa Burundi, Akbar Muderi.
Kipindi cha pili kilirejea kwa kasi huku Rayon ikiendelea kulisakama lango la wapinzani wao. Jitiada hizo ziliza matunda dakika ya 57 wakati Ibrahim Djingarey alipopachika bao la pili na kuamsha shangwe kubwa kutoka kwa mashabiki waliokuwa wamefurika uwanjani.
Jamus SC, ambayo imekuwa moja ya timu zilizoshangaza wengi kwenye michuano ya mwaka huu, ilipambana kurudi mchezoni na kufanikiwa kupata bao la kufuta machozi dakika ya 70 kupitia kwa Bandjouhou.
Hata hivyo, matumaini ya Jamus SC kusawazisha yalizimwa kabisa dakika ya 86 baada ya Gloire Tambwe kumalizia shambulio kali la kushtukiza na kuifungia Rayon Sports bao la tatu lililohitimisha ushindi huo wa mabao 3-1.
Vita ya Fainali na Zawadi Nono za Fedha
Kwa matokeo hayo, fainali ya CECAFA Kagame Cup 2026 sasa itakuwa kati ya Rayon Sports na Gor Mahia, huku Jamus SC ikitarajiwa kushuka dimbani kuwania nafasi ya tatu dhidi ya Al Hilal ya Sudan.
Mbali na heshima ya kutwaa ubingwa wa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, timu zitakazofanya vizuri zitajinyakulia kitita kikubwa cha fedha:
-
Bingwa (Nafasi ya 1): Dola 30,000 za Marekani (Tsh Milioni 79.3)
-
Mshindi wa Pili (Nafasi ya 2): Dola 20,000 za Marekani (Tsh Milioni 52.9)
-
Mshindi wa Tatu (Nafasi ya 3): Dola 10,000 za Marekani (Tsh Milioni 26.4)