Baraket Hmidi Aondoka Azam FC, Rejea Stade Tunisien
Aliyekuwa winga wa Azam FC, Baraket Hmidi, amekamilisha rasmi usajili wake wa kujiunga na Klabu ya Stade Tunisien ya nchini kwao Tunisia kwa ajili ya msimu wa 2026-2027.
Hmidi (23), alijiunga na Azam FC Agosti 16, 2025, akitokea CS Sfaxien ya Tunisia na kusaini mkataba wa miaka miwili uliopangwa kumalizika Juni 30, 2027. Hata hivyo, baada ya kuudumu kikosini hapo kwa msimu mmoja pekee, pande zote mbili zimefikia makubaliano ya kuachana.
Licha ya matarajio makubwa wakati anasajiliwa, winga huyo alikabiliwa na ushindani mkali wa namba kutoka kwa wachezaji wa kikosi cha kwanza kama Idd Seleman ‘Nado’, Mzee Hassan Mzee, na Abdul Suleiman ‘Sopu’.
Kutokana na ukosefu wa nafasi ya kucheza, uongozi wa Azam FC ulimtoa kwa mkopo kwenda Diyala SC ya Iraq wakati wa dirisha dogo la usajili la Januari 2026. Baada ya kumalizika kwa msimu wa 2025-2026, nyota huyo alirejea kikosini kabla ya kuachwa rasmi na kurudi nchini kwao Tunisia.
Katika kipindi cha miezi sita aliyoitumikia Azam FC, Hmidi alichangia pasi moja ya bao (assist) kwenye Ligi Kuu, wakati Azam FC ilipoifunga Mbeya City mabao 2-0 mnamo Septemba 24, 2025.
Urejeo wa mawinga Kipre Junior kutoka MC Algiers ya Algeria na Gibril Sillah kutoka Al-Ahly SC Benghazi ya Libya umeongeza ushindani kikosini, hatua iliyochochea zaidi maamuzi ya Hmidi kuondoka na kujiunga na Stade Tunisien.