Katiba ya Simba SC: BMT Yatoa Msimamo Mzito Utekelezaji Mabadiliko
Baraza la Michezo la Taifa (BMT) limeweka wazi kuwa jukumu la kutekeleza Katiba iliyorekebishwa ya Simba SC pamoja na kukamilisha mabadiliko yaliyopitishwa na wanachama ni la klabu hiyo, huku likisisitiza kuwa Serikali tayari ilikamilisha wajibu wake wa kuidhinisha na kukabidhi katiba hiyo.
Msimamo huo umetolewa kupitia taarifa rasmi kwa umma na Katibu Mtendaji wa BMT, Neema Msitha, ikieleza kuwa Katiba hiyo ilipitishwa na Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Simba mnamo Novemba 30, 2025, kabla ya kuwasilishwa kwa Msajili wa Vyama na Vilabu vya Michezo kwa ajili ya uchambuzi wa kisheria.
Baada ya kukamilika kwa uchambuzi huo, BMT kupitia Msajili iliidhinisha na kuikabidhi rasmi Simba Katiba hiyo mnamo Februari 18, 2026, ili ianze kutumika rasmi.
Msitha amebainisha kuwa hatua hiyo ilikamilisha kikamilifu wajibu wa Serikali, hivyo kuanzia wakati huo jukumu la kuhakikisha Katiba inatekelezwa linabaki ndani ya Klabu ya Simba.
“Utekelezaji wa maamuzi yaliyomo katika Katiba hiyo haupaswi kufanywa na Serikali kwa niaba ya Klabu,” alieleza Msitha, akisisitiza kuwa maamuzi hayo ni ya wanachama wenyewe kupitia Mkutano Mkuu.
Hata hivyo, BMT imeeleza kuwa Serikali iko tayari kuisaidia Simba pale yatakapojitokeza masuala ya kiutaratibu yanayohitaji ufafanuzi, ikizingatiwa mipaka na mamlaka ya kila taasisi.
Kutokana na hatua hiyo, Serikali imeitaka Simba kutumia vyombo na taratibu zake halali kukamilisha utekelezaji wa Katiba hiyo, huku ikiahidi kuendelea kusimamia maendeleo ya michezo nchini kwa kuzingatia sheria, uwazi, na uwajibikaji.