Yammy Ametangaza Kuvunjika kwa Uhusiano Wake na Ahmed: “I’m Single”
Yammy Athibitisha Kuwa ‘Single’, Amwaga Ahmed Baada ya Miezi Chache ya Mapenzi Moto Moto
Mwanamuziki unaochipukia kwa kasi katika kiwanda cha Bongo Fleva, Yasirun Yasin Shaban, maarufu kama Yammy, ameweka wazi kuwa kwa sasa yupo huru na hana mahusiano ya kimapenzi baada ya kumaliza rasmi uhusiano wake na aliyekuwa mpenzi wake, Ahmed.
Yammy ametangaza habari hiyo kupitia ukurasa wake wa Instagram, akiwafahamisha mashabiki na wafuasi wake kuwa safari yao ya mapenzi imefikia kikomo. Kauli hiyo imekuja kufuatia kipindi cha hivi karibuni ambapo wawili hao walionekana kuwa karibu sana katika matukio mbalimbali ya kijamii.
“I’m single na sina mahusiano ya kimapenzi na aliyekuwa mwenza wangu, haya waja, dua zenu zimetimia,” aliandika Yammy kupitia mtandao huo.
Kutoka Kifichoni Mpaka Hadharani
Uhusiano wa Yammy na Ahmed uliingia kwenye gumzo kubwa baada ya msanii huyo kuanza kuonyesha viashiria vya mapenzi bila kumuweka wazi mhusika. Mfano mzuri ni wakati wa Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day), ambapo Yammy alionyesha zawadi kemkem pamoja na kiasi kikubwa cha fedha alichodai kupewa na mpenzi wake, ingawa hakumtaja jina.
Hata hivyo, kadiri siku zilivyokwenda, mambo yalianza kuwa wazi. Mwezi Julai, wawili hao waliamua kuweka wazi mahusiano yao na kuanza kuonekana pamoja hadharani kama wapenzi.
Ahmed Kwenye Video ya ‘Wasiwasi’ na Matukio ya Kijamii
Mapenzi yao hayakuishia uraiani tu, bali yaliingia hadi kwenye kazi ya muziki. Ahmed alionekana kama mhusika mkuu kwenye video ya wimbo wa Yammy unaokwenda kwa jina la “Wasiwasi”, uliotoka mwishoni mwa mwezi Julai. Kitendo hicho kiliwafanya mashabiki kuamini kuwa wawili hao walikuwa wamejenga msingi imara wa mahusiano yao.
Mbali na muziki, walionekana pamoja katika sherehe za kijamii, ikiwemo sherehe ya ‘baby shower’ ya msanii Zuchu, ambapo walishirikiana kutoa zawadi ya fedha.
Kimya Cha Ahmed na Sababu za Kuvunjika
Licha ya tangazo hilo la Yammy lililoamsha hisia tofauti miongoni mwa mashabiki, msanii huyo hakuweka wazi chanzo au sababu zilizopelekea kuachana kwao. Hali kadhalika, upande wa Ahmed bado haujatoa kauli yoyote kuhusiana na tangazo hilo.