CECAFA Wanawake 2026: Yei Joint Stars, Mafunzo SC na Rayon Sports Kukiwasha Kigali
Kipenga cha kuanza kwa Mashindano ya Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Wanawake kinapulizwa rasmi leo Ijumaa, Agosti 21, jijini Kigali, Rwanda.
Miamba ya soka la wanawake kutoka ukanda huu inaanza vita ya kusaka tiketi moja pekee ya kuwakilisha Afrika Mashariki kwenye michuano mikubwa zaidi ya klabu barani Afrika. Tanzania Bara inawakilishwa na Mabingwa Simba Queens, huku Mafunzo SC wakibeba bendera ya Zanzibar kwa mara yao ya kwanza kabisa.
Yei Joint Stars Vs Denden FC (Saa 7:00 Mchana)
Pambano la ufunguzi la Kundi A litazikutanisha Yei Joint Stars ya Sudan Kusini na Denden FC kutoka Eritrea katika Uwanja wa Kigali Pele, majira ya saa saba mchana kwa saa za Afrika Mashariki.
Yei Joint Stars ineingia kwenye mchezo huu ikiwa na uzoefu mkubwa, ikiwa ni mara yao ya sita kushiriki michuano hii ingawa bado hawajafanikiwa kucheza fainali. Kwa upande wa Denden FC, hii ni mara yao ya pili baada ya kushiriki mwaka 2025 jijini Nairobi na kuishia hatua ya makundi.
Rayon Sports Vs Mafunzo SC (Saa 10:00 Jioni)
Mchezo mwingine unaosubiriwa kwa hamu katika kundi hilo utazikutanisha wenyeji Rayon Sports ya Rwanda dhidi ya wageni wa mashindano, Mafunzo SC ya Zanzibar, majira ya saa kumi jioni kwenye uwanja huo huo.
Rayon Sports, ambao walifika fainali mwaka 2025 kabla ya kufungwa bao 1-0 na JKT Queens ya Tanzania, wanahitaji ushindi wa mapema nyumbani ili kujiweka vizuri.
Kwa upande wa Mafunzo SC, huu ni mtihani mkubwa lakini wa kihistoria. Akizungumzia maandalizi yao, kiungo mshambuliaji wa Mafunzo SC, Zainab Dotto, ameeleza utayari wa kikosi chao:
“Tunajua ni mechi ngumu sana kwa sababu hii ni mara wetu ya kwanza kucheza michuano hii. Lakini tunaamini kwa maandalizi tuliyoyafanya na maelekezo ya makocha wetu, tutapambana na kufanya vizuri.”
Mfumo Wa Mashindano Kundi A linaundwa na timu nne: Rayon Sports, Yei Joint Stars, Mafunzo SC na Denden FC. Ni timu mbili pekee zitakazomaliza kileleni ndizo zitakazofuzu hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo inayotarajiwa kuhitimishwa Agosti 31, 2026.