Habibu Kondo Bandari Tanzania
Habari za michezo

Habibu Kondo Kutimiza Maajabu ya Azam FC Bandari Tanzania? Ligi Kuu Inanukia!

Vardo August 26, 2026 8:49 am

Wakati watoza shuru wa Bandari Tanzania wakiendelea kujifua vikali kujiandaa na ushindani wa Ligi ya Championship msimu ujao, Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Habibu Kondo, ametoa kauli nzito akisisitiza lengo lake kuu ni kuipandisha timu hiyo kucheza Ligi Kuu Bara.

Bandari Tanzania inajiandaa kushiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza baada ya kufanya kweli na kupanda daraja kutoka First League. Ili kuhakikisha ndoto zao zinatimia, timu hiyo imeweka kambi Mtwara huku ikijihakikishia usajili wa nyota wenye majina makubwa na uzoefu wa soka la ushindani nchini.

Kati ya majina mazito yaliyotua kikosini hapo ni pamoja na aliyewahi kuwa beki wa Yanga, Joyce Lomalisa, pamoja na wachezaji wengine wenye uzoefu mkubwa kama Sixtus Sabilo, Mohamed Kassim, Ally Ramadhan, Razack Shekimweli, William Elias, Seleman Omary ‘Boban’, Hajji Ugando, Issah Ngoah, Ayoub Semtawa na Geofrey Kiggi.

Akizungumza kuhusu maandalizi ya timu hiyo, Kondo ameeleza kuwa usajili uliofanyika umezingatia ubora na mahitaji halisi ya timu na wala sio tu kuangalia majina ya wachezaji.

“Hatujaangalia majina tu bali hata ubora wa mchezaji na kiwango chake. Naamini kwa mipango yetu na mapenzi ya Mungu tunaweza kupanda Ligi Kuu, kwani ninayo historia ya kufanya hivyo nilipokuwa Azam FC mwaka 2008,” amesema Kondo.

Ili kutengeneza utimamu wa mwili na muunganiko mzuri wa kikosi chake, kocha huyo amepanga kucheza mechi kadhaa za kirafiki dhidi ya timu zenye ushindani mkubwa jijini Dar es Salaam kabla ya ligi kuanza.

Kondo amekiri kutambua ugumu wa Championship kutokana na kuwepo kwa timu kongwe na zenye uzoefu kama KMC, Mtibwa Sugar, Tanzania Prisons na Rhino Rangers, lakini amesisitiza kuwa wamejipanga ipasavyo kuhakikisha hawakwami njiani.

Rekodi Mbaya ya Ramadhan Chalamanda Mbele ya Yanga SC Sofia Ramadhani: Bondia wa Kike Anayetishia Amani Ulingoni Tanzania