Zuchu Jeshi la Mtu Mmoja: Akimbiza Rekodi ya YouTube Afrika Mashariki
Mwaka 2005, mwanamuziki wa Hip Hop, Fid Q, alitokea kwenye ngoma yake ‘Mwanza’ iliyotayarishwa na P-Funk Majani (Bongo Records) na kujitambulisha kama jeshi la mtu mmoja. Alionyesha kuamini katika uwezo wake binafsi—ujumbe uliojirejelea pia kwenye albamu yake ya kwanza, Vina Mwanzo Kati na Mwisho, iliyomwezesha kutwaa tuzo yake ya kwanza ya TMA.
Leo hii, mstari huo unamwelezea vyema mwimbaji wa WCB Wasafi, Zuchu. Kutokana na kasi yake na namba anazopata kwenye soko la muziki, Zuchu ni jeshi la mtu mmoja anayezidi kutawala Bongofleva.
Kutoka ‘Wana’ Mpaka Kileleni
Tangu alipotambulishwa rasmi mwaka 2020 kupitia wimbo Wana, Zuchu ameendelea kujenga himaya yake kwenye muziki wa Afrika Mashariki. Uandishi wake makini, uwasilishaji mwepesi, na midundo inayovutia vimekuwa nguzo kuu za mafanikio yake, huku akiwa mwanamuziki wa pili wa kike kusainiwa WCB Wasafi baada ya Queen Darleen.
hivi karibuni, Zuchu ameandika rekodi mpya baada ya video ya wimbo wake Kwikwi (2022) kufikisha tazamo (views) zaidi ya milioni 100 kwenye mtandao wa YouTube. Wimbo huo wa Amapiano/Afrobeats uliotayarishwa na S2kizzy unakuwa wimbo wake wa pili kufikisha idadi hiyo.
Rekodi Asiyokuwa Nayo Diamond Platnumz
Ngoma ya kwanza ya Zuchu kufikisha views milioni 100 ilikuwa Sukari (2021) mnamo Machi 2024, na kumfanya kuwa msanii wa kwanza wa solo Bongofleva kufanya hivyo kabla ya Jeje ya Diamond kuungana naye Agosti 2024.
Kwa sasa, Zuchu ndiye msanii wa kwanza Tanzania na Afrika Mashariki kuwa na nyimbo mbili za solo (bila kushirikisha msanii mwingine) zenye tazamo wa zaidi ya milioni 100 YouTube.
Hii ni rekodi ambayo hata bosi wake, Diamond Platnumz, hana! Wala Rayvanny, Harmonize, au Jux hawajaifikia. Nyimbo nyingine zilizovuka namba hizo nchini zilikuwa za ushirikiano (collaboration), kama vile Yope Remix, Inama, Waah!, na Kwangwaru.
Takwimu za Zuchu YouTube na Tuzo
-
Jumla ya Views: Zaidi ya bilioni 1.25 (Msanii wa kike anayeongoza Afrika Mashariki).
-
Nafasi Tanzania: Anashika nafasi ya 4 kwa jumla ya views nyuma ya Harmonize, Rayvanny, na Diamond.
-
Tuzo: Baada ya EP yake I Am Zuchu (2020), alishinda tuzo ya AFRIMMA kama Msanii Bora Chipukizi (2020) na baadaye Msanii Bora wa Kike Afrika Mashariki (2022).
Bila shaka, mtoto huyu wa nguli wa Taarab Khadija Kopa anaendelea kuthibitisha kuwa uwezo na juhudi zake binafsi ndivyo vinavyomweka kwenye kilele cha muziki wa Afrika.