Steve Barker Awajibu Wasiowasi: Simba Bado Inatengeneza Nafasi
Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, amewatoa hofu mashabiki wa timu hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Coastal Union, akisisitiza kuwa kiwango walichoonyesha uwanjani kilistahili matokeo makubwa zaidi.
Mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliopigwa katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuyo, Mbweni, Dar es Salaam, ulishuhudia Simba ikitawala mchezo kwa asilimia kubwa, ingawa iliondoka na pointi tatu kupitia bao hilo moja pekee.
“Hana Presha” – Barker Aeleza Mchezo Ulivyokuwa
Akizungumza baada ya mchezo, kocha huyo raia wa Afrika Kusini alisema kikosi chake kilitengeneza nafasi nyingi za wazi, na kwamba changamoto kubwa ilikuwa ni kutoingiza mpira nyavuni.
“Nadhani wewe na watu wengine mna wasiwasi zaidi kuliko mimi. Tumefanya kila kitu uwanjani. Kipa wao alifanya seivu nzuri na wakati mwingine mpira ulikuwa unatolewa kwenye mstari wa goli. Leo tungeweza kufunga mabao matano au sita,” alisema Steve Barker.
Barker aliongeza kuwa Coastal Union haikuweza kuleta tishio lolote kwenye lango la Simba kote katika dakika 90 za mchezo.
“Namna tulivyotawala mchezo ilikuwa ya kipekee. Sidhani kama walipata hata kona moja, wala siwezi kukumbuka faulo ya hatari au shuti lililolenga lango letu. Sikumbuki Kassali akiwa na kazi kubwa leo.”
Takwimu za xG na Mwelekeo wa Wachezaji Wapya
Kocha huyo alibainisha kuwa takwimu za nafasi za kufunga (Expected Goals – xG) zilionyesha Simba ilipaswa kuondoka na mabao manne hadi matano.
Amesisitiza kuwa mfumo wake ukiendelea kukaa sawa na wachezaji wapya kuelewana, safu ya ushambuliaji itaanza kutoa mabao mengi zaidi.
-
Uzoefu na Mfumo: Wachezaji kama Kalesto na Dumbia wakizidi kuingia kwenye mfumo, umaliziaji utaimarika.
-
Uchezaji Bora: Chilambo ameonyesha kiwango cha juu na kuleta urahisi katika utengenezaji wa nafasi.
-
Malengo ya Timu: Jambo la msingi kwa sasa ni kuendelea kupata pointi tatu kwenye kila mchezo.
Tathmini ya Mwalimu
Barker alitimisha kwa kueleza kuwa kwenye mpira kuna siku timu inatawala na kupata bao moja pekee, lakini kuna siku inatengeneza nafasi chache na kuondoka na mabao matatu au manne. Kwa upande wake, ushindi huo unaonyesha Simba ipo kwenye njia sahihi.