Mngqithi Afichua Hali ya Kikosi cha Yanga na Majeraha Botswana: “Fred Ngoma Yupo Kwenye Mashaka”
BOTSWANA: Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuthibitisha kuwa kikosi chake kipo katika hali nzuri kimwili na kisaikolojia kuelekea mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) dhidi ya Gaborone United.
Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho Jumamosi nchini Botswana kuanza rasmi kampeni yake ya kimataifa, ikisaka matokeo chanya ugenini kabla ya kuwakaribisha wapinzani wao katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mazoezi ya timu hiyo, Mngqithi alieleza kuwa wachezaji wengi wamerejea katika kiwango bora cha utimamu wa mwili na kuonyesha mwitikio mkubwa katika mipango ya benchi la ufundi.
“Mazoezi yamekwenda vizuri sana. Wachezaji wamepona kikamilifu na utimamu wao wa mwili uko juu. Mwitikio waliouonyesha katika siku hizi mbili za mwisho za maandalizi unatupa matumaini makubwa kuelekea mchezo wa kesho,” alisema Mngqithi.
Hali ya Majeraha Kikosini
Pamoja na utulivu huo, kocha huyo raia wa Afrika Kusini alibainisha kuwa kikosi chake hakijapata majeraha mapya kutoka kwenye mazoezi ya hivi karibuni. Hata hivyo, alifichua changamoto moja kuu katika eneo la kiungo.
Kiungo Fred Ngoma bado yupo kwenye shaka kubwa ya kuanza katika mchezo huo kutokana na kuendelea na programu ya kuuguza jeraha lake.
“Hatuna majeraha mapya kutoka kwenye haya mazoezi ya hapa Botswana, lakini tulisafiri tukiwa na Fred Ngoma ambaye bado anaendelea kupona polepole. Hajafikia kiwango cha kuwa tayari asilimia 100, hivyo ni mchezaji ambaye tuna shaka naye kama ataanzia kikosi cha kwanza,” aliongeza kocha huyo.
Kutokuwa tayari kwa Ngoma kunaweza kumlazimisha Mngqithi kufanya marekebisho kidogo kwenye safu yake ya kiungo ili kuhakikisha timu inashikilia umiliki wa mpira na kuhimili presha ya wenyejio wao.
Kwa Wananchi, mchezo huu wa ugenini ni hatua muhimu ya kuweka msingi thabiti wa kutinga hatua inayofuata, huku benchi la ufundi likipania kurudi nyumbani na faida ya mabao au pointi tatu muhimu.