Yanga vs Gaborone United: Zimbwe Jr Aweka Wazi Vita ya Alama 3
BEKI wa kushoto na nahodha msaidizi wa Yanga, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, amesisitiza kuwa kikosi chao kipo tayari kupigania ushindi dhidi ya Gaborone United ya Botswana, huku akibainisha kuwa maandalizi yote yameenda kama ilivyopangwa na sasa lengo ni kuvuna alama tatu.
Yanga inaanza kampeni yake ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) kwa kumenyana na Gaborone United katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali nchini Botswana. Mabingwa hao wa Tanzania Bara wanalenga kupata matokeo mazuri ugenini ili kujiweka kwenye nafasi nzuri kabla ya mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam.
Akizungumza kuelekea pambano hilo, Zimbwe Jr alisema hali ya kambi nchini Botswana ni shwari na wachezaji wote wapo tayari kutekeleza mbinu za benchi la ufundi.
“Tunaona ni wakati sasa wa kupata alama tatu muhimu kutokana na mazoezi tunayofanya hapa Gaborone. Kila kitu kinaenda vizuri tangu tulipowasili, tunamshukuru Mungu,” alisema Zimbwe Jr.
Beki huyo aliongeza kuwa nidhamu ya mchezo na kujituma kwa 100% ndivyo vitu vitakavyowapa matokeo chanya katika mchezo huo wa kwanza.
“Walimu wametukumbusha umuhimu wa kujitoa kwa sababu huu ni mchezo wa kwanza. Katika michezo hii miwili, ni lazima tuhakikishe tunamaliza kazi hapa ugenini ili mechi ya marudiano iwe rahisi kwetu,” aliongeza.
Ushindi ugenini utakuwa hatua kubwa kwa Wananchi katika safari yao ya kutafuta tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.