Chama Avunja Ukimya Simba SC: “Mbio za Ubingwa Bado Ndefu, CAF CL Lengo ni Makundi”
Kiungo mchezeshaji wa Simba SC, Clatous Chama, amewataka mashabiki na wadau wa soka kutojisahau kufuatia mwanzo mzuri wa msimu, akisisitiza kuwa mbio za kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara bado ni ndefu na zenye ushindani mkubwa.
Simba SC imeanza msimu kwa kasi ya kuvutia baada ya kukusanya pointi 15 katika michezo mitano ya kwanza. Licha ya matokeo hayo ya kuridhisha, Chama anaamini ni mapema mno kutoa tathmini ya jumla ya ubingwa.
“Ligi ni Ngumu na Yenye Mabadiliko” Akizungumzia mwenendo wa ligi, Chama alibainisha kuwa umakini unahitajika katika kila mchezo kwani ushindani ni mkubwa.
“Ni mapema kujumlisha hali ya ushindani kwa sababu tumecheza michezo mitano tu. Kushinda michezo yote ni jambo zuri na tunaimani ya kuendeleza wimbi hili. Lengo letu kuu msimu huu ni kurejesha taji la Ligi Kuu,” amesema Chama.
Aliongeza kuwa changamoto ya ligi inahitaji nidhamu ya hali ya juu:
“Ni ngumu sana kushinda ligi kwasababu michezo ni mingi. Leo unaweza kushinda, kesho ukatoka sare. Jambo la msingi kwetu ni kubaki na umakini na kutopoteza malengo.”
Kipimo cha Kimataifa: Lengo ni Hatua ya Makundi CAF Mbali na mikakati ya ndani, Chama amezungumzia mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF Champions League) dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi utakaopigwa katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Baada ya mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Malawi, kiungo huyo raia wa Zambia ameeleza kuwa kipaumbele chao cha kwanza ni kuhakikisha wanaingia hatua ya makundi kabla ya kuwaza hatua za mbele zaidi.
“Kwa sasa lengo letu kuu ni kufuzu hatua ya makundi. Tukishatimiza hilo ndipo tutakapozungumzia hatua zinazofuata. Kikosi kipo tayari na tuna hamu ya kufanya vizuri Jumapili hii nyumbani.”
Wito kwa Wanasimba Chama amehitimisha kwa kutoa rai kwa mashabiki wa Simba SC kujitokeza kwa wingi uwanjani kuipa timu hamasa:
“Nawaalika Wanasimba wote waje kwa wingi Uwanja wa Uhuru. Tutakuwa nyumbani na tunahitaji sapoti yenu yote ili kupata matokeo chanya.”