Bodi ya Filamu Tanzania
Burudani

Irene Uwoya na Mastaa A-List Bodi ya Filamu Tanzania

Vardo September 10, 2026 5:26 pm

Ujio wa mastaa wakongwe wa filamu nchini—Irene Uwoya, Jacqueline Wolper, Aunt Ezekiel na Kajala Masanja—katika ofisi za Bodi ya Filamu Tanzania mnamo Septemba 7, 2026, umeendelea kuibua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii kutokana na muonekano wao wa kipekee.

Mastaa hao wa kipindi maarufu cha A-List walifika katika ofisi hizo wakiwa wamevalia suti za kifahari na kujipamba kwa ustadi. Tofauti na ilivyozoeleka kwa watu wanaokwenda kuitikia wito wa taasisi za kiserikali, mastaa hao waliteremsha zulia jekundu (red carpet) nje ya jengo hilo na kupita juu yake kabla ya kuingia ndani.

Akizungumzia tukio hilo, Irene Uwoya alieleza kuwa uamuzi wao wa kuvaa suti haukuhusiana na shinikizo la wito huo, bali ni muendelezo wa mtindo wao wa maisha wa kupenda utanashati.

“Suti ni utanashati tu. Sisi siku zote huwa smart, sio kwamba tumevalia suti kwa sababu tumeitwa sehemu kama baadhi ya watu wanavyodai. Sio sababu tumeitwa sehemu basi twende kinyonge au wachafu,” alisema Uwoya.

Alipoulizwa kuhusu sababu za kuja na zulia jekundu na kulitandaza kabla ya kuingia, Uwoya alijibu kwa kicheko kifupi na kuomba aachwe bila kutoa maelezo zaidi.

Kwa upande wa Bodi ya Filamu Tanzania, Katibu Mtendaji Dk. Gervas Kasiga alibainisha kuwa kikao hicho kililenga kutoa onyo na kuwakumbusha wasanii hao wajibu wao wa kimaadili. Dk. Kasiga alieleza kuwa kipindi cha A-List kinaangaliwa na vijana wengi wanaowachukulia kama mfano wa kuigwa, hivyo ni muhimu maudhui yao yakazingatia maadili ya kitanzania.

Kipindi cha A-List huwakutanisha Uwoya, Wolper, Aunt Ezekiel na Kajala wakijadili maisha yao ya binafsi, kazi, urafiki na masuala mbalimbali yanayozunguka tasnia ya burudani.

Selemani Mwalimu Afunguka Ushindani Yanga, Aweka Wazi Malengo Yake Fei Toto Agoma Kuzungumzia Yanga na Simba, Aweka Wazi Mkataba Wake Azam FC