Manqoba Mngqithi Aivizia Simba: Ametamani Dabi Nyingine ya Kariakoo Kupiga “Msumari” Mwingine
Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, ametangaza wazi kuwa anatamani kukutana tena na wajadi wao, Simba SC, katika Dabi ya Kariakoo ili kupata fursa nyingine ya kuonyesha ubora wake na kuwapa furaha mashabiki wa Wananchi.
Mngqithi ameeleza kuvutiwa na ushindani, presha pamoja na hamasa kubwa inayozunguka pambano hilo linaloteka hisia za wapenda soka nchini Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla.
Kocha huyo raia wa Afrika Kusini tayari alipata ladha ya kwanza ya Dabi baada ya kuiongoza Yanga kuichapa Simba bao 1-0 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii uliopigwa Agosti 12, 2026, visiwani Pemba—ushindi uliopatikana kupitia bao la mshambuliaji Albert Kangwanda katika dakika ya 32.
Hata hivyo, Mngqithi hakujiridhisha na matokeo hayo pekee; anaangazia zaidi mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara uliopangwa kufanyika Oktoba 19, 2026, ambapo anaimani utakuwa kipimo kingine kizito kwa kikosi chake kuendeleza utawala dhidi ya Msimbazi.