Selemani Mwalimu Yanga
Yanga SC

Selemani Mwalimu Afunguka Ushindani Yanga, Aweka Wazi Malengo Yake

Vardo September 10, 2026 5:18 pm

Mshambuliaji wa Yanga SC, Selemani Mwalimu, ameweka wazi kuwa yuko tayari kutumia vyema kila fursa atakayopewa na benchi la ufundi kupambana kwa uwezo wake wote, huku akisisitiza kuwa ushindani mkubwa uliopo kikosini unampa hamasa ya kuzidisha juhudi.

Mwalimu ameeleza kuwa malengo makubwa ya klabu hiyo msimu huu pamoja na uwepo wa wachezaji wenye viwango vya juu si kitu kinachomkatisha tamaa, bali kinampa nguvu mpya ya kuendelea kujituma ili kuisaidia timu kufikia malengo yake.

“Ninapata nguvu kwa hiyo nitapambana. Nikipata nafasi nitapambana na nitajitolea kwa ajili ya timu,” alisema Mwalimu.

Vita ya Mataji Yote Msimu Huu

Akimulika malengo ya Yanga kwa msimu huu, mshambuliaji huyo alibainisha kuwa klabu hiyo haijajipanga kushindania Ligi Kuu ya NBC na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika (CAF Champions League) pekee, bali ipo tayari kusaka kila taji lililopo mbele yao ikiwemo Kombe la Shirikisho (FA Cup).

Amesisitiza kuwa huo ndio utamaduni wa Yanga, na wachezaji wote wameungana kuhakikisha wanaipigania klabu hiyo ili kutwaa mataji yote ya ndani na kufika mbali zaidi kimataifa.

“Malengo ya timu siyo tu Ligi Kuu na CAF Champions League, bali ni kuchukua makombe yote tunayoshiriki, kama Shirikisho na mashindano mengine ya msimu huu. Kwa hiyo wachezaji kwa ujumla tunashirikiana vizuri na tunapambana kwa kadri ya uwezo wetu,” aliongeza.

Upendo na Ushirikiano Ndani ya Yanga

Mwalimu hakusita kuwasifu mashabiki wa Yanga kwa ushirikiano na sapoti kubwa wanayotoa kwa timu hiyo, akieleza kuwa hayo ndiyo mafuta yanayowafanya wachezaji wapambane kwa jasho na damu uwanjani.

Aliongeza kuwa kikosi chote kinatambua wajibu wao wa kuweka furaha kwenye nyuso za mashabiki, na ndio maana wanalazimika kuongeza juhudi ili kuepuka matokeo yanayoweza kuwakatisha tamaa.

“Unajua katika mpira mchezaji kazi yake ni kufanya kazi. Yanga ni timu ambayo ina upendo mkubwa, kuanzia mashabiki, wachezaji na benchi la ufundi. Sapoti yao inatupa nguvu kubwa kwa sababu tunajua wako nyuma yetu,” alihitimisha Mwalimu.

Manqoba Mngqithi Aivizia Simba: Ametamani Dabi Nyingine ya Kariakoo Kupiga “Msumari” Mwingine Irene Uwoya na Mastaa A-List Bodi ya Filamu Tanzania