Kazi Bado! Kocha Wa Simba Atoa Onyo Kali Kuelekea Marudiano Ya Ligi Ya Mabingwa
MSHAMBULIAJI hatari wa Simba SC, Ibrahim Doumbia, ni miongoni mwa nyota wanaoelekeza nguvu zote kwenye mazoezi maalumu kuelekea mchezo wa marudiano wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mighty Wanderers ya Malawi.
Mchezo huo wa kukata na shoka utapigwa kesho Jumapili, Septemba 13, katika Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam. Simba inaingia uwanjani ikiwa na faida ya ushindi wa bao 1-0 iliyoupata katika mchezo wa kwanza uliochezwa nchini Malawi—bao lililowekwa kimani na mshambuliaji Anicet Oura katika dakika ya 65.
Licha ya ushindi huo wa ugenini, Kocha Mkuu wa Simba, Steve Barker, amesisitiza kuwa vita bado haijaisha na amewataka wachezaji wake kuingia uwanjani kwa umakini mkubwa.
Maandalizi ya Kikosi na Kauli ya Kocha
Barker anaendelea kukiwasha kikosi chake kwa kuwajenga kimbinu nyota wengine kama Clatous Chama, Elie Mpanzu, na Libasse Gueye ili kurekebisha makosa yaliyoonekana kwenye mchezo wa kwanza.
“Wapinzani wetu wanatambua kwamba wamepoteza mchezo wa kwanza, hivyo wanakuja wakiwa na shauku kubwa ya kupata ushindi. Tunawaheshimu kutokana na ubora wao, lakini lazima tutambue kuwa kazi bado inaendelea,” alisema Barker.
Kocha huyo aliongeza kuwa benchi la ufundi limefanyia kazi mapungufu yote na kwamba Simba haitauchukulia mchezo huo kwa wepesi.
“Makosa yaliyopita tunayafanyia kazi ili kuwa bora zaidi. Hauwezi kuwa mchezo rahisi. Matokeo ya dakika 90 za kesho ndiyo yatakayoamua nani anafuzu. Bado hatujafuzu, lakini tunapambana kuhakikisha tunatimiza malengo yetu,” aliongeza.
Simba inalenga kutumia vyema faida ya uwanja wa nyumbani na support ya mashabiki ili kulinda ushindi wao na kukata tiketi ya kusonga mbele katika michuano hiyo mikubwa zaidi kwa vilabu barani Afrika.