Arsenal Yaiwinda Saini ya Nico Paz: Tetesi za Usajili Ulaya Leo
Mabingwa wa England, Arsenal, wanafuatilia kwa karibu maendeleo ya kiungo mshambuliaji wa Como, Nico Paz (22). Kocha Mikel Arteta yupo kwenye mpango wa kuimarisha kikosi chake kwa kusajili viungo wenye ubora na uwezo wa kudumu kwa muda mrefu.
Paz, raia wa Argentina, amekuwa mmoja wa wachezaji wanaong’ara zaidi kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) chini ya kocha Cesc Fabregas. Kiwango chake kimevutia klabu kadhaa kubwa barani Ulaya.
Ingawa Como ilimsajili Paz kwa takriban Euro milioni 60, Real Madrid iliweka kipengele cha kumrejesha Santiago Bernabeu kwa Euro milioni 80 mnamo kiangazi cha mwaka 2027. Kipengele hiki kinaweza kuwa kikwazo kwa Arsenal, kwani Real Madrid inaweza kutumia haki hiyo hata kama Arsenal itafikia makubaliano na Como.
Fabregas amewahi kumfananisha Paz na Lionel Messi kutokana na urahisi wake wa kukabiliana na mabeki. Kwa upande wake, Paz alisema alichagua kubaki Italia ili kupata muda mwingi wa kucheza badala ya kurejea Madrid kugombea namba na viungo waliopo.
TETESI NYINGINE ZINAZOTREND ULAYA
-
Cher Ndour (Fiorentina): Kiungo huyu mwenye umri wa mwaka 22 anawindwa kwa karibu na Liverpool pamoja na Aston Villa kutokana na ukomavu na nguvu zake katikati ya uwanja.
-
Geny Catamo (Sporting CP): Sunderland inaendelea kufuatilia saini ya winga huyu wa Msumbiji (25). Catamo ameonyesha kiwango bora kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya akifunga bao moja katika ushindi wa 3-1 dhidi ya Galatasaray.
-
Lamine Camara (Monaco): Monaco inatarajia kupata Euro milioni 70 kutoka kwa Chelsea au Liverpool zinazowania saini ya kiungo huyu wa Senegal (22), baada ya mpango wake wa kwenda Chelsea kuvunjika siku ya mwisho ya usajili.
-
Lukas Nmecha (Leeds United): Mshambuliaji huyu wa Ujerumani (25) anatarajia kuondoka Leeds United mwishoni mwa msimu mkataba wake utakapomalizika, au hata katika dirisha la mwezi Januari kutokana na kukosa nafasi ya kucheza.
-
Luke Chambers (Liverpool): Celtic inafuatilia maendeleo ya beki huyu wa kushoto (22) ikiwa na mpango wa kumsajili mwezi Januari kupata huduma yake.
-
Wilfried Zaha: Winga huyu wa Ivory Coast (33) amepewa fursa ya kujiunga na Malaga baada ya kuondoka Galatasaray kama mchezaji huru kufuatia vipindi viwili vya mkopo klabuni Charlotte FC.
-
Raphinha (Barcelona): Barcelona inaandaa mkataba mpya hadi mwaka 2030 kwa ajili ya winga wake wa Brazil (29), licha ya mkataba wa sasa kumalizika mwaka 2028.
-
Hamza Abdelkarim (Barcelona): Miamba hiyo ya Hispania imekamilisha mkataba mpya wa mshambuliaji huyu wa Misri (18) hadi mwaka 2030, ukiwa na kipengele cha kuvunja mkataba kwa Euro milioni 150.
-
Gabriel Rajkovic (Valerenga): Arsenal na Chelsea zinaongoza mbio za kumsajili kinda huyu wa Norway (15) ambaye tayari anacheza kikosi cha kwanza cha Valerenga na kuvunja rekodi kadhaa Ulaya.