Kocha AbdulSaleh: JKU Imeanza Kuwa Bora ZPL, Alenga Kurekebisha Safu ya Ushambuliaji
KOCHA Mkuu wa JKU, AbdulSaleh Mohammed amebainisha kuwa kikosi chake kimeanza kuonyesha kiwango bora baada ya kuibuka na ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Wembe, mchezo uliopigwa kwenye Uwanja wa Mao A, Unguja.
Baada ya kucheza mechi tatu za Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), JKU imefanikiwa kukusanya pointi saba kufuatia ushindi wa mechi mbili na sare moja. Timu hiyo haijapoteza mchezo wowote hadi sasa huku ikiwa ndiyo kinara wa ufungaji ligini ikiwa imeweka kimani mabao manane na kuruhusu matatu pekee.
Akizungumzia mchezo huo, kocha AbdulSaleh amesema ingawa walilenga kupata mabao mengi zaidi, walitambua mapema kuwa mechi isingekuwa nyepesi kutokana na maandalizi ya wapinzani wao.
“Tulitambua wazi mechi haitakuwa rahisi kwetu, hivyo tulijua watakuja wakiwa wamejipanga na mechi itakuwa ngumu. Ndiyo sababu iliyotufanya tuhitaji kufunga mabao mengi mapema,” alisema AbdulSaleh.
Kocha huyo aliongeza kuwa Wembe walitumia mbinu ya kukaa nyuma sana kuanzia eneo la katikati ya uwanja, hali iliyowalazimu JKU kutumia maeneo ya pembeni kutengeneza mashambulizi ya kushtukiza.
Hata hivyo, amekiri kuwa bado wana changamoto katika umaliziaji wa nafasi wanazotengeneza kutokana na kumkosa mshambuliaji mwenye uwezo wa kutumia makosa ya wapinzani kikamilifu—kosa ambalo ameahidi kulifanyia kazi haraka kabla ya mechi zinazofuata.