Simba SC Yaichapa Mighty Wanderers 6-1, Yatinga Hatua Inayofuata Ligi ya Mabingwa Afrika
Klabu ya Simba SC imetinga hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo baada ya kuishushia kipigo kizito cha mabao 6-1 Mighty Wanderers ya Malawi katika mchezo wa marudiano uliopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam. Ushindi huo umezifanya Msimbazi kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 7-1.
Mchezo huo wa marudiano uliingia uwanjani ukiwa na presha ndogo kwa Simba SC iliyokuwa imeshinda bao 1-0 katika mechi ya kwanza nchini Malawi. Hata hivyo, Wekundu wa Msimbazi waliaza mchezo kwa kasi ya juu na kutawala idara zote kuanzia dakika ya kwanza.
Chama na Gueye Wawasha Moto Uwanja wa Uhuru
Clatous Chama alianza kuifungulia Simba ushindi mapema kwa kufunga bao la kwanza dakika ya 7 kabla ya kuongeza la pili dakika ya 33. Mshambuliaji Libasse Gueye naye alionyesha kiwango cha juu baada ya kupachika bao dakika ya 27 na kuiweka Simba katika nafasi nzuri.
Mighty Wanderers walipata bao la kufutia machozi dakika ya 44 kupitia mkwaju wa penalti uliowekwa kimiani na Isac Kaliati, na kufanya timu hizo kwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa mabao 3-1.
Kipindi cha Pili: Mauaji Yanaendelea
Kipindi cha pili kilipoanza, Simba SC iliendelea kushambulia bila huruma. Libasse Gueye alikamilisha usiku wake kwa kufunga bao lake la pili (bao la 4 kwa Simba) katika dakika ya 69.
Akitokea benchi, Kalesto Makgalwa aliongeza bao la tano dakika ya 88, kabla ya Morice Abraham kuhitimisha karamu hiyo ya mabao kwa kufunga la sita dakika ya 90.
Hatua Inayofuata: Kibarua Dhidi ya 15 de Agosto
Baada ya kuiondoa Mighty Wanderers kwa jumla ya mabao 7-1, Simba SC sasa inaelekeza nguvu zake katika hatua inayofuata ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo itakabiliana na 15 de Agosto kutoka Equatorial Guinea.