Juma Masoud Afunguka Alivyochelewa Songea United, Aomba Muda Aunde Kikosi cha Maangamizi
Kocha Mkuu wa Songea United inayoshiriki Ligi ya Championship, Juma Masoud, amewataka mashabiki na wadau wa klabu hiyo kuwa wavumilivu na kumpa muda zaidi wa kutengeneza timu itakayoweza kushindana kikamilifu katika msimu wa 2026-2027.
Masoud amebainisha kuwa kuchelewa kuanza kwa maandalizi ya msimu (Pre-Season) kumetokana na baadhi ya wachezaji kuchelewa kuripoti kambini, hali iliyokwamisha mipango ya mapema ya kikosini hapo.
Akizungumza kuhusu mwenendo wa timu hiyo inayotokea Songea mkoani Ruvuma, kocha huyo aliyewahi kuinoa FGA Talents (sasa Fountain Gate) alisema:
“Tuna maingizo mapya ya wachezaji kwa ajili ya msimu mpya na taratibu tumeanza kutengeneza muunganiko mzuri wa kiuchezaji. Ligi ya Championship ni ngumu sana, na ili kuendana na ushindani wake ni lazima tujipange mapema iwezekanavyo.”
Kipimo cha Masoud na Rekodi Zake
Kocha Masoud alijiunga na Songea United Januari 2026 akichukua nafasi ya Meja Mstaafu, Abdul Mingange. Tangu kuwasili kwake, amekuwa akipambana kuirejesha timu hiyo katika ubora wake kuanzia mchezo wake wa kwanza dhidi ya Rhino Rangers.
Hii si mara ya kwanza kwa Masoud kuonyesha uwezo kwenye Ligi ya Championship:
-
Msimu wa 2024-2025: Akiwa na Stand United, aliiongoza kumaliza katika nafasi ya 3 ikiwa na pointi 61 na kufanikiwa kucheza mechi za mchujo (‘Play-Off’) za kusaka tiketi ya kupanda Ligi Kuu Bara.
-
Kwenye Play-Off: Stand United ilianza kwa kuitupa nje Geita Gold kwa jumla ya mabao 4-2, kabla ya kukwamishwa na Fountain Gate kwa jumla ya mabao 5-1 katika hatua ya mwisho.
Kwa uzoefu alionao kwenye ligi hiyo, Masoud anaamini kuwa muda alioomba ukipatikana, Songea United itakuwa moja ya timu tishio zaidi msimu huu.