Bernard Kamungo
Michezo

Bernard Kamungo: Kutoka Kambi ya Nyarugusu Mpaka Soka la Kulipwa Marekani

Vardo September 21, 2026 9:52 am

Wakati watu wengi wakitumia mtandao wa YouTube kuangalia video za vichekesho na burudani ya muziki, mambo yamekuwa tofauti kwa winga Mtanzania, Bernard Kamungo. Nyota huyo anayekipiga kunako klabu ya FC Dallas nchini Marekani, alitumia mtandao huo kama chombo kikuu cha kujifunza lugha ili kuendana na mazingira mapya.

Kamungo, ambaye alikulia katika Kambi ya Wakimbizi ya Nyarugusu mkoani Kigoma, Tanzania, anafichua kuwa kuwasili kwake Marekani kulimpa wakati mgumu kutokana na kikwazo cha lugha.

“Lugha ninazozijua ni Kiswahili kwa sababu niliishi Tanzania kwenye Kambi ya Nyarugusu na Kifaransa kwa sababu baba yangu anatokea DR Congo. Nilikuwa napata tabu sana, lakini nilipambana na kujifunza Kiingereza,” alisema Kamungo.

YouTube na Mazingira Vikawa Shule Yake

Akiwa anatafuta njia za haraka za kuandana na maisha ya Marekani, Kamungo aliamua kutumia mitandao ya kijamii, hasa YouTube, kama darasa lake la kujifunza Kiingereza. Njia hiyo, pamoja na ushirikiano wa kila siku na wenzake, ilimsaidia kwa kiasi kikubwa kumudu lugha hiyo kwa haraka.

Kutokea Chini Mpaka Ligi Kuu (MLS)

Maisha ya soka ya Kamungo nchini Marekani yalianza kupata mwelekeo alipojiunga na North Texas (2021/22) inayoshiriki Ligi Daraja la Tatu. Akiwa hapo, alionyesha kiwango cha juu baada ya kufunga mabao 22 katika michezo 52.

Kiwango hicho kilimfungulia milango ya kujiunga na FC Dallas inayoshiriki Ligi Kuu (MLS). Katika msimu huu:

  • Amecheza dakika 1,230 katika mechi 16.

  • Ameweka rekodi ya kutoa asisti 4.

  • FC Dallas imeshinda michezo 8, sare 1 na kupoteza 4 pekee pindi Kamungo anapoanza kwenye kikosi cha kwanza.

Kutokana na mchango wake mkubwa, Januari 7, 2025, FC Dallas ilimuongezea mkataba mpya utakaomweka klabuni hapo hadi mwisho wa msimu wa 2027, huku ikiwa na kipengele cha kuongeza hadi 2029.

Wito Taifa Stars

Kutokana na uwezo wake unaozidi kuimarika, winga huyo mwenye umri wa miaka 24 amejumuishwa kwenye kikosi cha Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) chini ya Kocha Miguel Gamondi, kujiandaa na mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Twanga Pepeta Kutua Mwanza: Bella, Nyoshi na Phina Kuwasha Moto Rock City Mall!