Kifo cha Mama Fatma Karume: Yanga Yalia na Msiba Mkubwa, Injinia Hersi Afichua Hili
Uongozi wa Klabu ya Yanga umeeleza kusikitishwa na kifo cha Mjumbe wa Baraza la Wadhamini wa klabu hiyo, Mama Fatma Karume, aliyefariki dunia jana, Septemba 21, 2026.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa Yanga imepokea msiba huo kwa huzuni na simanzi kubwa, huku ikimtaja marehemu Mama Fatma Karume kama mmoja wa viongozi waliotoa mchango uliotukuka katika maendeleo na ustawi wa klabu hiyo kongwe nchini.
Kauli ya Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said
Akizungumzia msiba huo mzito, Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema klabu hiyo imepoteza kiongozi mwenye busara, hekima na aliyekuwa na mapenzi ya dhati kwa Yanga.
“Huu ni msiba mkubwa sana kwetu. Tumepoteza kiongozi mkubwa mwenye busara, hekima na mapenzi ya dhati na klabu yetu,” amesema Injinia Hersi.
Mchango Wake Katika Ardhi ya Makao Makuu Jangwani
Akiangazia historia na mchango wa marehemu, Hersi aliongeza kuwa miongoni mwa mambo makubwa ambayo Yanga haitamsahau nayo Mama Fatma Karume ni mchango wake wa kipekee katika kufanikisha upatikanaji wa ardhi yaliyojengwa makao makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa Twiga na Msimbazi, Jangwani jijini Dar es Salaam.
“Tutamkumbuka Mama yetu Fatma Karume kwa mengi mazuri aliyofanya ndani ya klabu yetu, ikiwemo upatikanaji wa ardhi ya jengo letu la makao makuu, Jangwani jijini Dar es Salaam. Hakika, tumempoteza mwanachama na moja ya nembo muhimu za klabu hii,” alisisitiza Rais Hersi.
Salamu za Pole
Kupitia taarifa yake rasmi, Yanga imetoa salamu za pole kwa familia ya marehemu, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na wadau wote wa michezo nchini Tanzania, huku ikiwaombea ustahimilivu na nguvu katika kipindi hiki kigumu cha majonzi.
“Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Ameen,” ilihitimisha taarifa ya klabu hiyo.