Lucas Kikoti Anena Mzito: Aipongeza Safu ya Yanga, Amchagua Maxi Nzengeli
Safu ya ulinzi ya Yanga SC imeendelea kuwa mwamba na kikwazo kikubwa kwa washambuliaji wengi msimu huu. Kiungo mshambuliaji mwenye uzoefu wa Namungo FC, Lucas Kikoti, amefunguka na kuweka wazi kuwa ukuta wa mabingwa hao watetezi ndio mgumu zaidi kukutana nao kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Hata hivyo, Kikoti amekiri kuwa mwanzo wa msimu kwake haukuwa mzuri kama alivyotarajia. Anafichua kuwa sababu kuu ilikuwa mapumziko marefu aliyoyapata nyumbani kabla ya kuanza kwa msimu, hali iliyomfanya achelewe kurejea kwenye kasi yake ya kawaida.
“Kwangu msimu haujaanza vizuri kwa sababu nilipata mapumziko marefu kabla ya msimu kuanza. Niliporudi nilikuwa bado najitafuta, lakini najisukuma ili nirudi kwenye kiwango changu. Malengo yangu ni kuisaidia Namungo ifike nafasi za juu na kufunga angalau mabao matatu msimu huu,” alisema Kikoti.
Ukuta wa Yanga SC Uvyo Msumbufu
Akitathmini safu za ulinzi alizokutana nazo kwenye Ligi Kuu Bara, Kikoti hakuchelea kuitaja Yanga SC kuwa ndiyo yenye mabeki waliokamilika zaidi.
Anasema ubora wa ukuta wa Yanga unatokana na uzoefu mkubwa walionao wachezaji wao kuanzia mabeki wa pembeni (full-backs) hadi mabeki wa kati, jambo linalowapa uwezo wa kusoma mchezo na kuzima mashambulizi kwa urahisi.
Mzuka wa Maxi Nzengeli na Upole Wao
Mbali na kuisifu Yanga, Kikoti alimchagua kiungo mshambuliaji wa timu hiyo, Maxi Nzengeli, kuwa mchezaji anayemvutia zaidi katika ligi kuu msimu huu.
Kikoti ameeleza kuwa kinachomkosha zaidi kutoka kwa Nzengeli ni roho ya kupambana na kujitoa kwa ajili ya timu. Pia alidokeza kuwa mashabiki wengi wamekuwa wakimfananisha naye kutokana na tabia yao inayofanana ya kuwa wapole wakiwa nje na ndani ya uwanja.
Mabadiliko ya Viwanja na Changamoto ya Ratiba
Kwa upande wa miundombinu, Kikoti amepongeza hatua iliyopigwa na Ligi Kuu Bara, akisema ubora wa viwanja vya sasa unasaidia sana kukuza kiwango cha soka ukilinganisha na miaka ya nyuma.
Hata hivyo, amebainisha kuwa ratiba ya ligi bado ni changamoto kubwa kwa ustawi wa wachezaji:
-
Mapumziko Marefu: Kucheza mechi moja pekee kwa mwezi kunashusha kiwango cha mchezaji na kupoteza mechi ‘fitness’.
-
Mrundikano wa Mechi: Mechi zinapofuatana kwa karibu mno huongeza uchovu mwingi na hatari ya majeraha.
Mbinu za Juma Mgunda na Mipango ya Namungo FC
Kuhusu mfumo wa usajili wa Namungo FC, Kikoti alisema timu yao tofauti na klabu zinazostawisha vijana, imejikita zaidi kwenye kusajili wachezaji wazoefu na wenye uwezo mkubwa ili kutengeneza ushindani wa namba.
Pia alimsifu Kocha Mkuu, Juma Mgunda, kwa kusimamia nidhamu na ushindani ndani ya kikosi:
“Kocha Mgunda anapenda sana ushindani. Alinishauri kama mchezaji mwenye uzoefu nijipange kisaikolojia na kitekniki ili kila ninapopata nafasi niitumie kikamilifu.”
Ujumbe Kuelekea Azam FC na Singida kwenye CAF
Kikoti hakuwa nyuma kuwapa ushauri wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya Kimataifa ya CAF (Azam FC na Singida BS), akisisitiza umuhimu wa kutumia kikamilifu faida ya viwanja vya nyumbani ili kutinga hatua ya makundi kabla ya kuwaza hatua zinazofuata.
Presha ya Kupambana Kujiokoa na Mipango ya Kustaafu
Akizungumzia hali ngumu ya matokeo ambayo Namungo imekuwa ikipitia, Kikoti alikiri kuwa vita ya kukimbia janga la kushuka daraja humnyima mchezaji amani na hata usingizi, huku ikileta msongo mkubwa wa mawazo.
Kuhusu maisha baada ya soka, kiungo huyo alifichua kuwa anatarajia kucheza kwa miaka miwili hadi mitatu zaidi kabla ya kutundika daluga.
Hata hivyo, hana mpango wa kuingia kwenye ukocha pindi atakapostafu. Badala yake, anataka kutumia muda wake mwingi kuwa karibu na familia yake baada ya miaka mingi ya kuwa mbali nao kutokana na kambi na safari za soka, huku akiwa tayari amewekeza kwenye nyumba, mashamba na elimu ya wadogo zake.